Ofisi ya Rais wa Nne wa Kenya inadai kuwa wafanyikazi hao hawajalipwa kwa muda wa miaka miwili.
Akizungumza wakati wa kikao na wanahabari siku ya Jumatatu, Msemaji wa ofisi hiyo Kanze Dena alisema hawezi kujumuisha kwa jumla ni kiasi gani hicho.
"Kwa bahati mbaya hatujapata mshahara kwa miaka miwili iliyopita. Sina uwezo wa kuhesabu ni kiasi gani ambacho rais wa zamani ameweza kutumia kwa sababu hiyo ni pamoja na mafuta, chakula tunachokula kama wafanyikazi, bili za usafiri, umeme. " Kanze alidai.
Akizungumza wakati wa kikao na wanahabari, Kanze alisema serikali pia imekataa kuwaongezea kandarasi wafanyakazi wawili.
Wafanyakazi aliosema ni Kanze Dena Mararo na msimamizi John Kariuki.
"Ofisi bado inasubiri uthibitisho na mawasiliano juu ya kwa nini walikataa kwa uwazi kuorodhesha kandarasi za wafanyikazi hawa wawili wa kitaalam," alisema.
Aidha alisema serikali haijafanya wala kuwezesha ukarabati wowote, matengenezo ya gari lolote wala haijatumia mafuta ya gari chini ya ofisi hii.
Katika kikao na wanahabari, Uhuru kupitia kwa msemaji wake Kanze Dena badala yake alisema kwa sasa anatumia magari aliyopewa kwa njia ya mpito.
Kanze alisema magari yanayotumika ni yale ambayo Uhuru aliondoka nayo kutoka Kasarani baada ya hafla ya kukabidhi MAMLAKA mnamo Septemba 2022.
"Baada ya mabadiliko hayo, mazungumzo kuhusu ununuzi wa magari hayo kama inavyotakiwa na Sheria yalianza kati ya ofisi hizo mbili...," Kanze alisema.