Watu sita waliopatikana na hatia ya mauaji ya aliyekuwa mbunge wa zamani wa Juja George Thuo watarajiwa kuhukumiwa hii leo.
Mahakama kuu ya Milimani mnamo Aprili mwaka huu iliagiza kuwa sita hao walishirikiana katika kumtilia sumu mbunge huyo kwenye klabu ya Porkies katika kaunti ya Kiambu.
Kisa hiki kilitukia mnamo mwaka 2013 ambapo mbunge huyo alitiliwa sumu ya wadudu aina ya cyhalothrine.
Sita hao ni: Esther Mulinge, Samuel Kuria Ngugi, Christopher Lumbazio, Ruth Watahi Irungu,Andrew Karanja Wainaina na Paul Wainaina Boiyo.
Wakati wa maendeleo ya kesi hii mnamo Mei 28, waendeshaji mashtaki walirai korti iwahukumu washukiwa adhabu ya juu zaidi.
Vilevile, waendeshaji hao walisisitiza kuwa washukiwa hao wasionyeshwe huruma kwani hawakuwa na majuto wakati wakishiriki uhayawani huu.
Mke wa hayati Thuo aliiambia korti kuwa mumewe alikuwa mwenye buheri wa afya kabla ya kupatana na washukiwa hao siku hiyo ya maafa.
“Alipopatiwa fursa ya kuzungumza, mkewe Thuo alimwambia hakimu Roseline Korir kuwa mumewe alikuwa na siha njema kabala ya kifo chake cha ghafla, ambacho kilifanyika akiwa pamoja na washukiwa hawa,” Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP) ilisema kwenye mashtaka.
