Maseneta wametoa kauli mseto katika vikao vya bunge la seneti Jumatano kuhusu ripoti ya kamati ya uwekezaji wa umma na fedha maalum katika kaunti katika kupiga msasa ripoti ya ukaguzi ya watoaji huduma za maji.
Wakati wa uwasilishaji ya ripoti hiyo, mwenyekiti wa kamati hiyo ambaye pia ni seneta wa kaunti ya Vihiga Godfrey Osotsi alisema kuwa alikuwa na furaha kuripotia seneti kuwa kamati yake imeweza kutatua migogoro ya utawala katika kampuni za za maji kwenye kaunti zote 47.
Wakati wa kujadili ripoti hiyo, seneta wa Nairobi Edwin Sifuna alisema kuwa kuna tuhuma nzito za ufisadi katika kampuni ya maji ya jiji la Nairobi. Seneta Sifuna alisema kwamba wafanyakazi wa kampuni hiyo ndio wafanyabiasharawa kuuza maji jijini.
Sifuna hata hivyo, aliitaka tume ya maadili na kupambana na ufisadi EACC kufuatilia kesi zilizowasilishwa awali ili kukomesha uhuni huo.
Seneta wa kaunti ya Mombasa Mohamed Faki naye alisikitikia kuwa kampuni ya kuwajibikia maswala ya maji taka katika kaunti yake, humwaga maji hayo katika bahari ya Hindi.
Seneta huyo alitaka kamati inayoongozwa na seneta Osotsi kurejea katika kaunti hiyo na kuangalia kwa umakini tatizo hilo.
Vile vile, seneta wa Makueni Dan Maanzo naye kwa upande wake amestaajabia namna siasa za maji zimekuwepo kuanzia wakati wa utawala wa rais mstaafu hayati Daniel Moi.
“Kutoka enzi za Moi mwaka wa 1986 nikiwa shule ya msingi, kulikuwa na mpango wa kila boma kuwa na maji safi. Kufikia leo, maji bado iko mbali na maboma mengi. Maji ya mabomba yangali kufikia maboma mengi nchini.” Alisema seneta Maanzo.
Seneta huyo ameitaka serikali kuu kuwekeza katika miradi ya maji kwanza kabla ya miradi mingine ya maendeleo kutekelezwa.
Katika ripoti iliyowasilishwa mbele ya seneti na kamati hiyo, ilibainika kuwa tatizo kuu linalozizonga kampuni za maji katika kaunti, ni usimamizi mbaya kutokana miundo dhaifu na bodi dhaifu.
Kamati hiyo ilipendekeza magavana kuajiri maafisa wakuu watendaji wa bodi za maji katika kaunti ambao wamehitimu ili kuhakikisha kampuni hizo zinaendesha kikamilifu huduma zao.