Maafisa wa usalama katika eneo la Kabale, Magharibi mwa nchi jirani ya Uganda wanamsaka shabiki mmoja wa Arsenal anayedaiwa kumshambulia shabiki mwenzake wa soka ambaye alishabikia wapinzani wao wakuu, Manchester United.
Tukio hilo linasemekana kutokea siku ya Jumapili jioni kufuatia sare ya 2-2 ya Arsenal na Liverpool katika mechi yao ya mkondo wa kwanza iliyochezwa kwenye Uwanja wa Emirates.
Kwa mujibu wa gazeti la Daily Monitor, tukio hilo lilitokea katika Kituo cha Biashara cha Kyobugombe katika Kata ndogo ya Kaharo, Wilaya ya Kabale.
Inaarifiwa kuwa marehemu Benjamin Okello alipoteza maisha baada ya mabishano makali na mshukiwa aliyetambulika kwa jina la Onan wakati wa kutazamwa kwa mechi na baada ya filimbi ya mwisho.
Walioshuhudia
wanadai kuwa malumbano yalizuka kufuatia bao la kusawazisha la Liverpool katika
dakika ya 81.
Shabiki wa Man United, Okello, alishindwa kuzuia furaha yake baadaya kushuhudia bao la kusawazisha la Liverpool na akaanza kusherehekea kwa furaha, jambo ambalo liliripotiwa kumkera Onan ambaye nio mfuasi sugu wa Arsenal. Mabishano yalizuka, yakazidi kwa haraka.
Kwa hasira, Okello alimrushia Onan popcorns alizokuwa ameshika, jambo ambalo lilisababisha makabiliano makali.
Baada ya mechi kumalizika, hali ilizidi kuwa mbaya na kugeuka kuwa ya vurugu. Hapo ndipo Onan anadaiwa kuokota fimbo na kumpiga Okello, na kumuacha akiwa amejeruhiwa vibaya.
Kamanda wa Polisi wa Wilaya hiyo Bw. Joseph Bakaleke, alisema mamlaka bado inaendelea kumsaka mshukiwa Onan ambaye amejificha kufuatia tukio hilo.
Mwenyekiti wa kata ndogo ya Kaharo LCIII Bw. Edmond Tumwesigye alifichua kuwa mshukiwa anaaminika kuwa na umri wa miaka 30 na ni mkazi wa mtaa mmoja na marehemu.