Waziri wa mazingira Aden Duale amehusisha kubanduliwa kwa Rigathi Gachagua na hulka yake ya kuwapiga vita watu wengi, wakiwemo wale wadogo ndani ya serikali ya Kenya Kwanza.
Akizungumza kwenye runinga ya Citizen usiku wa Jumatano, Duale alisema kwamba Gachagua alipoteza dira yake pale alipowekeza sana katika kujitengenezea maadui wengi wa kisiasa kuliko marafiki.
Mbunge huyo wa zamani wa Garrisa Mjini alisema kwamba haijawahi tokea katika historia ya bunge kuona idadi kubwa hivyo ikipiga kura kumbandua mwanasiasa, akilinganisha idadi hiyo na maadui ambao Gachagua alijitengenezea katika kipindi chake kifupi kwenye ofisi ya naibu rais.
“Rais wa sasa aliwasilisha hoja ya kumfungulia mashitaka alipokuwa Waziri wa Kilimo, lakini kushtakiwa kwake kuligeuka kuwa kura ya imani. Alizungumza kwa saa mbili, na wanachama (wabunge) 115 walimuunga mkono,” Duale alisema akikumbuka kuwa alikuwa mmoja wa wabunge hao mwaka 2009.
Kwa mujibu wa Duale, Gachagua aliwekeza nguvu nyingi kuwapiga vita hata maafisa wadogo wa serikali akiwemo Dennis Itumbi na Farouk Kibet, msaidizi wa kibinafsi wa rais Ruto.
"Ukiniuliza, ni vizuri kuwekeza kwa marafiki, na nadhani DP huyo wa zamani aliwekeza zaidi katika kupigana na watu kutoka ngome yake, ikiwa ni pamoja na watu wadogo kama Dennis Itumbi na Farouk Kibet. Unapokuwa mkubwa, usijishushe, bakia tu juu,” Duale alisema.
Duale aliangazia zaidi umuhimu wa kukuza urafiki wa kisiasa, akisisitiza jinsi mbinu ya Gachagua ilivyofanya kazi dhidi yake wakati wa kura ya kuondolewa madarakani.