RAIS William Ruto ametangaza kuwa serikali yake ina
mpango wa kupanuliwa kwa barabara kuu ya kutoka Nairobi kuelekea Nakuru mwaka
ujao.
Akizungumza wakati wa ibada katika kanisa la AIC
Kipkorgot mjini Eldoret siku ya Jumapili, Rais aliwahakikishia Wakenya kuhusu
kujitolea kwa serikali kuboresha njia kuu za uchukuzi.
Kiongozi huyo wa taifa alitoa tamko hilo la matumaini
jijini Eldoret, wakati ambapo mamia ya Wakenya wanaotumia barabara hiyo kuelekea
nyumbani Krismasi wamekwama kwenye msongamano mkubwa.
Ruto alifafanua zaidi kwamba upanuzi wa njia hiyo ya
uchukuzi hapo awali itaanzia Barabara Kuu ya Nairobi-Nakuru, na mipango ya
kuipanua hadi Malaba, Kaunti ya Busia kuendelea baadae.
"Ahadi
ninayotaka kuwapa ni kwamba mwaka ujao tutaanza ujenzi wa njia mbili za kubebea
mizigo kutoka Nairobi, kwanza hadi Nakuru na kisha kutoka Nakuru baadaye
tutaipeleka Malaba," Ruto alisema.
Ruto alifichua kuwa makubaliano ya awali ya Ubia kati ya
Sekta ya Umma na Kibinafsi (PPP) na kampuni ya Ufaransa ya kujenga Barabara Kuu
za Nairobi-Nakuru yalikuwa yameshindikana.
Rais Ruto aliendelea kueleza kuwa mipango mbadala inafanyiwa
kazi.
"Tulikuwa na Mpango wa PPP kati yetu na kampuni ya Ufaransa,
lakini haukufaulu. Hata hivyo, tuna njia nyingine mbadala ambazo tunafanyia
kazi kama serikali,” Rais alisema.
Rais alisisitiza umuhimu wa mradi huo katika kupunguza
msongamano wa magari na kuimarisha ufanisi wa usafiri katika njia hiyo ambayo
huwa na shughuli nyingi.
"Tayari tuna mpango na tuko kwenye majadiliano na kampuni tofauti
kuhusu jinsi barabara hiyo itafanywa ili tuweze kupunguza msongamano na kutoa
uwezo zaidi wa usafiri kwa miundombinu yetu," Ruto alieleza.
Barabara kuu ya Nairobi-Nakuru-Malaba ni kiungo muhimu kati
ya Kenya na majirani zake katika eneo la Afrika Mashariki, kuwezesha biashara
na harakati.
Rais Ruto pia alisisitiza maendeleo ya kiuchumi ya Kenya,
akitaja mfumuko mdogo wa bei, kuongezeka kwa mauzo ya nje, na usalama wa
chakula nchini.

