ALIYEKUWA kiongozi wa kundi haramu la Mungiki, Maina Njenga amejitokeza na kuonekana kupingana vikali na wito wa aliyekuwa naibu raia Rigathi Gachagua kuhusu kuunganisha eneo pana la Mlima Kenya.
Njenga ambaye sasa anaonekana kutetea uongozi wa rais
William Ruto anasisitiza kwamba kuondolewa kwa Gachagua serikalini hakumaanishi
kwamba eneo zima la Mlima Kenya limeondoka serikalini na kuingia katika mrengo
wa upinzani.
“Ningependa
kuambia nchi nzima ya Kenya kwamba kuondolewa kwa bwana Rigathi Gachagua sio
kuondolewa kwa eneo la Mt Kenya. Eneo la Mlima Kenya litasalia imara na tisti
na hatutayumbishwa hata kidogo,” Njenga alisema.
Njenga alisisitiza kwamba si rahisi kwa eneo hilo
kujiondoa katika serikali ya rais Ruto kwani karibia asilimia 50 walimpigia
kura ya urais.
“47%
ya watu wa Mt Kenya walipia hii serikali kura. Na hiyo ndio sababu William Ruto
ndiye rais kwa sasa. Na ni vizuri kwetu kuwa ndani ya serikali kuliko kuipiga
vita kutoka nje. Kama kuna vita yoyote ambayo tunaenda kupigana basi
tutaipigana tukiwa ndani,’ alisema.
Kauli ya Njenga inakuja wakati ambapo inasubiriwa kuona
Gachagua akitangaza mweneleo wake mpya wa kisiasa baadae mwezi huu.
Kiongozi huyo alisisitiza kwamba kuondolewa kwa
Gachagua serikalini kama naibu rahisi hakuna uhusiano wowote na maslahi ya eneo
hilo pana bali ni kwa sababu ya kutokea kutoelewana kibiashara baina yake na
viongozi wengine ndani ya serikali ya Ruto.
“Ninajua
kwamba kumekuwa na uadui mwingi, kwa sababu ya mwanamume mmoja ambaye
aliondolewa serikalini kwa sababu ya sababu zake mwenyewe. Hakuondolewa serikalini
kwa sababu ya masilahi ya Mlima Kenya, ni kwa sababu ya biashara ambazo
walikuwa wanafanya na viongozi wengine serikalini,”
Njenga alisema.
