KATIBU mkuu wa muungano wa wafanyikazi nchini COTU, Francis Atwoli ameibua cheche za kisiasa baada ya kuwazomea baadhi ya wanasiasa wanaojikusanya tayari kumtoa rais Ruto ofisini katika uchaguzi wa 2027.
Akizungumza Januari 28 na waandishi wa habari, Atwoli alisema
kwamba wanasiasa wote ambao wanahaha juu na chini kwa lengo la kumshinda Ruto
wanafanya kazi bure, akisema kuwa siasa za Kenya hazishindwi kuzungumzia
mahitaji ya wakenya bali kwa kujikusanyia watu kimaeneo.
Atwoli alisema kwamba hata Fred Matiang’i – waziri wa zamani
wa usalama wa ndani ambaye anapigiwa debe na baadhi ya Wakenya hawezi kuwa
rais, akimtaja kuwa mtoza ushuru mbaya zaidi hata kuliko rais Ruto mwenyewe.
“Mnataka kuniambia Matinag’i
anaweza kuwa rais wa jamhuri ya Kenya? Mimi mwenyewe nimefanya kazi na Matiang’i.
Yeye ni mtoza ushuru, zaidi ya William Ruto. Mimi namjua,” Atwoli alisema.
Alidai kwamba waziri huyo wa zamani hakuwahi mpigia kampeni
hata siku moja mgombea wa upinzani Raila Odinga kuelekea uchaguzi wa 2022 licha
ya kuwa bosi wake Uhuru Kenyatta ndiye alikuwa anaongoza kampeni za Odinga.
“Wakati tulikuwa katika
Azimio na tulikuwa tunatoka, Matinag’i hakuwahi hata mpigia kampeni Raila. Hakuonekana
mahali popote akimpigia debe Raila. Walikuwa bize katika ofisi ya rais
wakitengeneza pesa. Mimi namjua kwa sababu nilikuwepo,” Atwoli alisisitiza.
Atwoli alisema kwamba hakuna Mkenya ambaye amepigania haki za
Wakenya zaidi kumliko na kueleza kwamba ingekuwa kura zingepigwa kwa msingi huo
basi yeye angekuwa rais.
“Kila Mkenya anajua
vizuri sana kwamba kama siasa za Kenya zilikuwa zinaamuliwa kwa masuala tata,
basi leo hii Atwoli angekuwa rais wa Jamhuri ya Kenya,” Atwoli alisema.
“Lakini ukweli ni kwamba
siasa za Kenya zimejikita katika ukabila,” aliongeza.
Mzee Atwoli alipuuzilia mbali uwezekano wa muungano mkubwa
zaidi kuundwa ili kumtoa Ruto mamlakani 2027 akisema kwamba Azimio ndio ulikuwa
muungano mkubwa kabisa lakini bado hawakufanikiwa kushinda urais.
“Nilikuwa ndani ya
Azimio, tulikuwa na muungano mkubwa zaidi kuliko ule ambao wanataka kuanzisha
sasa lakini tukashindwa,” alifoka.