WAZIRI wa utumishi wa umma Justine Muturi kwa mara nyingine tena ameonekana kulenga mkuki wake kwenye kifua cha serikali haswa akikosoa vikali mauaji ya waliotekwa nyara.
Akizungumza katika hifadhi ya maiti
ya City alipofika kwa ajili ya vijana wawili kati ya watatu waliotekwa nyara
Mlolongo mwishoni mwa mwaka jana na baadae kupatikana wakiwa maiti, Muturi
alisema kwamba ni jambo la kusikitisha sana kwa vijana hao kupatikana maiti.
Waziri huyo alisisitiza kwamba si jambo
la kufurahisha kuona juhudi za wiki kadhaa za kuwatafuta vijana hao kuishia
kwenye hifadhi ya maiti.
Waziri huyo alisema kwamba ni wakati
wa taifa kwa jumla kuweka pembeni shughuli zozote zinazoendelea ili kuelekeza
nguvu na juhudi katika kuangazia suala la utekaji nyara ambalo limekuwa gumzo
la kitaifa katika miezi ya hivi karibuni.
“Nafikiri ni wakati sasa nchi
iweke kando shughuli zingine zozote na kuelekeza nguvu katika suala la utekaji
nyara na mauaji ya kinyama,” Muturi
alisema.
Alisisitiza kwamba licha ya kuwepo
ndani ya serikali, hana Habari yoyote kama kunayo kanuni yoyote inayounga mkono
utekaji nyara wa aina yoyote.
Muturi alisema kwamba si jambo la
kufurahisha kuona wazazi wakiwatafuta wapendwa wao kwa Zaidi ya siku 40 na mtu Fulani
ameketi mahali akiwaambia kuhusu kutafuta utatuzi wa suala la kiuchumi.
“Si poa kwamba wazazi wanaweza
kukaa kwa kipindi cha Zaidi ya siku 40 kuwatafuta wanao wapendwa na tunaketi
mahali tukidai kwamba tunajadili masuala ya uchumi wa nchi, uchumi kwa nani?”
Muturi alihoji.
“Kama tunawateka nyara na
kuwaua Watoto, sasa ni nani tunajadilia uchumi huo? Suala hili linastahili
kushughulikiwa na uharaka unaostahili,” aliongeza.
Tamko la Waziri huyo linajiri siku
moja tu baada ya miili ya vijana wawili kati ya 3 waliotekwa nyara Mlolongo –
Justus Mutuma na Martin Mwau kupatikana katika makafani ya City.