
RAIS William Ruto ametoa ahadi ya kipekee kwa wanafunzi wa shule za msingi katika kaunti ya jiji la Nairobi.
Kama njia moja ya kupiga jeki mpango ulioanzishwa na gavana
Sakaja wa kutoa mlo shuleni kwa wanafunzi maarufu ‘Dishi na Kaunti’, rais Ruto
alisema kwamba yuko tayari kuongeza mlo wa chapati katika safu ya vyakula
hivyo.
Akizungumza wakati wa ziara yake ya maendeleo katika kaunti
ya Nairobi, Ruto aliahidi wanafunzi kwamba atanunua mashine ya kupika chapati
hadi milioni moja kwa ajili yam lo wao shuleni.
Alimtwika gavana Sakaja jukumu la kutafuta mashine hiyo ya
kipekee ambayo itakuwa inapika chapati milioni moja kutosheleza idadi ya
wanafunzi wanaofaidika na mpango wa Dishi na Kaunti.
“Gavana ameniuliza ya kwamba ili tuongeze chapati kwa Dishi ya Nairobi, ninunue mashine ya kutengeneza chapo (chapati), na nimekubali nitanunua mashine ya kutengeneza chapati. Sasa wewe gavana tafuta mahali ya kununua mashine ya kutengeneza chapati milioni moja,” Ruto alisema huku wanafunzi wakimshangilia.
Kiongozi wa nchi alianza ziara yake ya maendeleo ya siku 5
katika kaunti ya Nairobi Jumatatu na alikuwa katika mtaa wa Eastleigh Eneobunge
la Kamukunji.
Ruto alitumia fursa hiyo ya kukutana na wananchi kupigia debe
mshikamano wake mpya na kiongozi wa ODM, Raila Odinga akisisitiza kwamba
kuungana kwao ni kwa ajili ya kuleta faida na maendeleo katika kila pembe ya
nchi.
Baadae leo Jumanne, Ruto anatarajiwa kuzindua ujenzi wa bweni
la vitanda 800 katika Shule ya Sekondari ya St Teresa’s iliyoko Mathare, eneo
la mapumziko kwa ajili ya ujenzi wa vyumba 12 vya madarasa katika Shule ya
Msingi ya Mabatini na kukagua ujenzi wa vyumba vya madarasa katika Shule ya
Sekondari ya Mathare Mchanganyiko.
Jumatatu, Ruto alizindua mradi wa Kukuza Upya wa Mto Nairobi,
ambao alidai utafaidika takriban vijana 30,000 kutoka Nairobi kupitia ajira,
kando na ujenzi wa masoko na nyumba za bei nafuu.