logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Zifahamu nchi zinazonyonga ukikutwa na dawa za kulevya

Kenya, hukumu ya kifo ilitekelezwa mara ya mwisho mwaka 1987 kufuatia jaribio la kuipindua serikali la 1982, ambapo Hezekiah Ochuka alinyongwa kwa kosa la uhaini.

image
na Davis Ojiambo

Habari18 March 2025 - 08:15

Muhtasari


  • Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International linakiri kuongezeka kwa visa vya watu kunyongwa katika utekelezaji wa adhabu ya kifo duniani kote.
  • Nchini Kenya, hukumu ya kifo ilitekelezwa kwa mara ya mwisho mwaka 1987 kufuatia jaribio la kuipindua serikali la 1982, ambapo Hezekiah Ochuka alinyongwa kwa kosa la uhaini.


Taarifa za adhabu ya kunyongwa kwa mwanamke Mkenya Margaret Macharia Nduta, imezagaa sana kuanzia mwishoni mwa wiki hii.

Mwanamke huyo alipatikana na hatia ya kukutwa na dawa za kulevya kilo mbili huko Vietnam na kuhukumiwa kunyongwa adhabu ambayo inapaswa kutekelezwa leo jioni. Hata hivyo hakuna uhakika kama utekelezaji wa adhabu hiyo umefanyika ama la, lakini Kenya iliingilia kati kutaka adhabu hiyo isitekelezwe.

Katibu Mkuu wa masuala ya kigeni Kenya, Korir Sing'oei alieleza kuzungumza na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Vietnam Nguyen Minh Hanga kuomba kuzuiwa kunyongwa kwa mwanamke huyo. Kwa mujibu wa Sing'oei waziri huyo wa Vietnam alimuhakikishia kuwa ombi hilo litazingatiwa.

Wakati sakata la Margaret likiwa hivyo, makala hii ni kukupa piacha kuhusu adhabu ya kunyongwa duniani kwa watu wanaohukumiwa kwa kesi za dawa za kulevya.

Kwa mujibu wa ripoti kuhusu adhabu ya kifo kwa makosa ya dawa za kulevya, 2023 kupitia Shirika lisilo la kiserikali (NGO) linalojitolea kupunguza athari mbaya za kiafya, kijamii na kisheria za matumizi ya dawa za kulevya na sera ya dawa, (HRI) inaonyesha kuwa nchi 16 duniani ziliripoti adhabu za kifo 375 zinazohusiana na dawa za kulevya, ikiwa ni ongezeka la asilimia 20% ukilinganisha na mwaka 2022.

Nchi hizo ni miongozi mwa nchi 34 ambazo bado zinatekeleza adhabu za kifo mpaka mwishoni mwa mwaka 2023, huku kikiwa na watu takribani 3000 duniani wanaosubiri kunyongwa kutokana na makosa ya dawa za kulevya, kwa mujibu wa ripoti hiyo.


Ukikutwa na dawa za kulevya katika nchi hizi unayongwa


Kuwa na sheria ya kunyonga ni jambo moja lakini kutekeleza adhabu yenyewe ya kunyongwa ni suala lingine. Zipo nchi nyingi ambazo zina sheria za adhabu za kunyonga mpaka kufa kutokana na makosa mbalimbali. Lakini ni nchi chache zinazowanyonga kweli watu waliokutwa na hatia na kupewa adhabu hiyo. Mara nyingi huendelea kukaa magerezani kwa muda mrefu, unaofanana kabisa na adhabu ya kifungo cha maisha.

Kukutwa na dawa za kulevya ni moja ya makosa makubwa yanayosababisha watu wengi kuhukumiwa kunyongwa. Kati ya makosa yote ya adhabu za kunyongwa mpaka kufa, makosa ya kukutwa na dawa za kulevya yanachukua asilimia 42%, karibu nusu, HRI linaripoti. Likiwa ni ongezeko kubwa zaidi katika kipindi cha hivi karibuni.

Nchi tano za China, Kuwait, Iran, Saudi Arabia na Singapore zenyewe zimeripoti kutekeleza adhabu hiyo ya kifo kwa mwaka 2023, kwa mujibu wa Shirika la HRI. Nchi ya Korea Kaskazini na Vietnam pia zinatajwa kutekeleza adhabu hiyo, kwa watuhumiwa wa dawa za kulevya, ingawa upatikanaji wa taarifa za idadi ya wanaonyongwa imekuwa na ugumu.

Katika nchi hizo watu 467 waliojihusisha na dawa za kulevya walinyongwa mpaka kufa katika mwaka 2023, ikiwa ni ongezeko la asilimia 44% ukilinganisha na mwaka 2022.

Juhudi za Kimataifa kuzuia adhabu ya kifo kwa dawa za kulevya zinafua dafu?

Sheria ya kimataifa inakataza matumizi ya hukumu ya kifo kwa makosa ambayo si ya makusudi na yanayoonekana "mabaya zaidi".

Licha ya jitihada za nchi kwa nchi, kama ilivyofanya Kenya kutafuta namna ya kuzuia raia wake Margaret asinyongwe Vietnam, kumekuwa na juhudi za kimataifa kuondoa adhabu hiyo kwa makosa ya dawa za kulevya. Juhudi ambazo hazijazaa matunda.

Mnamo 1988, Umoja wa Mataifa ulifanya uchunguzi ili kubaini uhusiano kati ya viwango vya hukumu ya kifo na mauaji. Matokeo yalitolewa mwaka wa 1996. Yalisema hivi: "Uchunguzi umeshindwa kutoa uthibitisho wa kisayansi kwamba kunyongwa kuna athari kubwa zaidi kuliko kifungo cha maisha.

Umoja wa Mataifa umekuwa ukisitiza kuwa makosa ya dawa za kulevya hayafikii kiwango hicho cha wakosaji kuhukumiwa kunyongwa. hilo linajidhihirisdha kwa baadhi ya nchi kuendelea kutekeleza adhabu hiyo ya kuwanyonga waliokutwa na hatia katika kesi za dawa za kulevya.

Singapore imekosolewa kimataifa baada ya kuanza tena matumizi ya adhabu ya kifo mnamo Machi 2022, kufuatia mapumziko ya miaka miwili wakati wa janga hilo.

Baadhi ya mauaji 11, yaliyotekelezwa kwa kunyongwa, yalifanyika mwaka huo, na takriban watu 16 walikuwa wamenyongwa kufikia Novemba 2023, kulingana na Human Rights Watch.

Miongoni mwa waliouawa ni Saridewi Djamani, mwanamke wa Singapore ambaye alipatikana na hatia ya ulanguzi wa dawa za kulevya mwaka wa 2018. Alikuwa mwanamke wa kwanza kunyongwa katika jimbo hilo kwa takriban miaka 20.

Kuwait yenyewe imeingia katika orodha ya kutekeleza adhabu ya kunyonga kwa waliokutwa na hatia katika kesi za dawa za kulevya, baada ya kufanya hivyo mwaka 2023, ikiwa ni kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2007.

Mwezi Julai, 2023, Pakistani yenyewe ilifuta adhabu ya kifo kwa makosa ya dawa za kulevya na kuwa nchi ya kwanza kufanya hivyo katika kipindi cha zaidi ya muongo mmoja.

Utekelezaji wa adhabu ya kifo kwa nchi za Afrika Mashariki


Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International linakiri kuongezeka kwa visa vya watu kunyongwa katika utekelezaji wa adhabu ya kifo duniani kote.

Kwa mujibu wa takwimu za hivi karibuni kuna visa 1,153 vya adhabu ya kunyongwa mwaka 2023 kwa ujumla, ongezeko la asilimia 31 kutoka 883 mwaka 2022. Ni idadi ya juu zaidi kunakiliwa na Amnesty International tangu 2015, wakati watu 1,634 walinyongwa. Hivi ni visa vya kunyongwa kwa ujumla.

Adhabu ya kifo haitumiki kabisa katika nchi 112, ikilinganishwa na 48 mwaka 1991. Nchi sita zilikomesha hukumu ya kifo kikamilifu, au kwa sehemu, mnamo 2022. Nne - Kazakhstan, Papua New Guinea, Sierra Leone na Jamhuri ya Afrika ya Kati - ziliifuta kabisa. Guinea ya Ikweta na Zambia zilisema itatumika tu kwa uhalifu mkubwa zaidi.

Mnamo Aprili 2023, bunge la Malaysia pia lilipiga kura ya kuondoa hukumu ya kifo ya lazima kwa makosa 11 makubwa ya uhalifu , yakiwemo mauaji na ugaidi. Bunge la Ghana lilipiga kura ya kukomesha kabisa hukumu ya kifo mnamo Julai 2023.

Kwa Afrika, adhabu ya kifo haitekelezwi sana, licha ya hukumu ya adhabu hiyo kutolewa.

Kwa mfano Tanzania, inatajwa kutotekeleza adhabu hiyo kwa miaka karibu 30, ingawa idadi ya walihukumiwa kunyongwa kwa makosa mbalimbali, ikivuka 600, kwa mwaka 2023.

Ingawa kosa la mauaji, linabeba idadi kubwa ya wanaohukumiwa kunyongwa Tanzania kuliko kukutwa na dawa za kulevya.

Nchini Kenya, hukumu ya kifo ilitekelezwa kwa mara ya mwisho mwaka 1987 kufuatia jaribio la kuipindua serikali la 1982, ambapo Hezekiah Ochuka alinyongwa kwa kosa la uhaini. Mwaka 2021, watu 601 walikuwa wamehukumiwa kifo na hukumu nyengine 14 za kifo zilitolewa mwaka huohuo. Hukumu nyingi hazikuwa za dawa za kulevya.

Nchini Uganda, Bunge la nchi hiyo lilipitisha sheria inayopinga hukumu ya adhabu ya kifo kwa baadhi ya uhalifu. Wakati huo kulikuwa na wafungwa wapatao 133 ambao walihukumiwa kunyongwa lakini ikipita zaidi ya miaka 20 bila kunyongwa ama kutekelezwa kwa adhabu hiyo.


Makala Zinazohusiana


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved