
NAIBU wa rais profesa Kithure Kindiki amefunguka ukweli kwamba tangu aapishwe kama naibu rais Novemba mwaka jana, kuna baadhi ya watu wamekuwa wakijaribu kuanzisha mzozo wa vita vya maneno na bosi wake, rais William Ruto.
Akizungumza katika shule ya Ng’arachi
katika kaunti yac Laikipia wakati wa siku ya kwanza ya ziara ya rais Ruto
katika eneo la Mlima Kenya, Kindiki alisema kwamba alipuuzilia mbali ushauri
huo na kuahidi kuwa naibu mtiifu kwa rais.
Kindiki alisema kwamba atakuwa naibu
mtiifu kwa rais katika kumsaidia majukumu ya kuhakikisha Kenya inafanikiwa
kulingana na ajenda za maendeleo ya serikali.
Alisema kwamba alikataa kuchukua
ushauri huo kwa vile yeye si kiongozi wa upinzani, kwani kazi ya kupinga rais
aliyeko madarakani na serikali yake ni ya mirengo ya upinzani.
“Mimi nataka nikuhakikishie nitakuwa
msaidizi mwema nyuma yako kwa ukakamavu na pamoja na wenzangu tunaenda
kuifikisha Kenya katika nchi ya ahadi chini ya uongozi wako.”
“Kuna watu naona wameanza
kunishauri-shauri, eti sijui ooh wewe hukai kama unapigana na rais vizuri,
sijui wewe hukai kama unabishana na rais…kwani tangu siku gani kazi ya DP ikawa
ya kupigana na rais? Kwani mimi ni kiongozi wa upinzani? Si mambo ya kupigana
na serikali ni ya wale watu wako nje ya serikali?” Kindiki alihoji.
Akitetea wajibu wake, Kindiki alisema
kwamba kazi yake kuu ni kumuunga mkono rais Ruto katika kutekeleza ajenda zake
za maendeoe kwa wananchi wa Kenya.
“Kazi yangu ni kumuunga rais mkono,
kumtetea na kufanya kazi chini yake na kwa kushirikiana na wenzangu tutafuata
chenye anafanya ili kufanikisha kwa wananchi,” Kindiki aliongeza.
Msomi huyo wa sheria alisema haya saa
chache baada ya rais Ruto kufichua jinsi ilikuwa vigumu kufanya kazi na
Gachagua kama naibu wake.
Katika mahojiano ya kipekee na
vyombovya habari vya Mlima Kenya usiku wa Jumatatu kutoka ikulu ndogo ya
Sagana, Nyeri, Ruto alifichua kwamba Gachagua hakuwahi muonyesha ushirikiano
katika kusukuma ajenda za serikali.
Ruto alidai kwamba Gachagua kwa wakati
mmoja alimtishia kumfanya rais wa muhula mmoja tu ikiwa hangetii takwa lake la
kumpa shilingi bilioni 10.