
ALIYEKUWA waziri wa utumishi wa umma Justin Muturi amevunja kimya chake, takribani wiki moja baada ya kufutwa kutoka kwa baraza la mawaziri.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya
habari, Muturi alidai kwamba anajua fika sababu iliyopelekea kibarua chake
kuota nyasi katika serikali ya rais William Ruto.
Mwanasheria mkuu wa zamani wa serikali
alisema kwamba huenda kufutwa kwake kulichochewa na misimamo yake mikali ambayo
amekuwa nayo dhidi ya utekaji nyara.
Mara si moja, Muturi amekuwa
akiinyooshea serikali kidole cha lawama kuhusu suala la utekaji nyara, akidai
kwamba asasi za kiusalama zimekuwa zikihusika.
“Hakuna siri kwamba nilifutwa kutokana
na msimamo wangu mkali dhidi ya utekaji nyara na mauaji na kile ambacho
kimeitwa kususia vikao vya baraza la mawaziri,” Muturi alisema.
Hata hivyo, spika huyo wa zamani wa
bunge la kitaifa alisema kwamba kama rais Ruto alidhani kumfuta ndio njia ya
kumnyamazisha, basi ameula wa chuya.
Aliapa kuendeleza misururu ya
mashambulidi dhidi ya serikali na kuitaka iwajibikie kile alichokitaja kuwa
matendo yao maovu dhidi ya wananchi.
“Lakini nathubutu kusema hivi, kama
lengo [la kufutwa] lilikuwa ni kuninyamazisha, kwa bahati mbaya wamebofya
nambari tofauti. Kwa sababu siwezi choka kupigania haki za watu wa hii Jamhuri,
bila kujali gharama yake,” Muturi alisema.
Hotuba yake inakuja siku moja tu baada
ya kukabidhi mamlaka ya ofisi aliyekuwa akiishikilia kwa waziri mwenye mamlaka
makuu, Musalia Mudavadi.
Rais Ruto juzi akizungumza na
wanahabari kutoka eneo pana la Mlima Kenya kuelekea mwanzo wa ziara ya siku 5
ya kimaendeleo katika eneo hilo, aligusia kuondolewa kwa Muturi katika baraza
la mawaziri.
Ruto alisema kwamba Muturi alijifuta
kazi mwenyewe kwani alianza kususia vikao vya baraza la mawaziri, akisema
kwamba hata kuondoka kwake hakutamuathiri pakubwa kwani bado ana pesheni kama
spika mstaafu.
Ruto alitangaza mabadiliko kwenye
baraza lake la mawaziri wiki jana ambapo alimteua mbunge wa Mbeere Kaskazini
Geoffrey Ruku kuchukua nafasi ya Justin Muturi katika wizara ya utumishi wa
umma.