logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Raila Amtaka Ruto Kuwasikiliza Wakenya Kwa Umakini Zaidi

Raila alisisitiza umuhimu wa kuweka maslahi ya taifa mbele ya tofauti za kisiasa, akihimiza njia ya pamoja katika uongozi wa nchi.

image
na Tony Mballa

Habari20 June 2025 - 16:44

Muhtasari


  • Aliyasema hayo wakati wa warsha ya Tatu ya Baraza la Mawaziri iliyoandaliwa na Rais William Ruto katika eneo la Karen, Nairobi.
  • Warsha hiyo ndiyo ya kwanza tangu ODM na UDA kusaini makubaliano ya ushirikiano (MOU) yenye lengo la kuimarisha ajenda ya utoaji huduma kwa kuzingatia maslahi ya wananchi.

Kiongozi wa ODM, Raila Odinga, ameitaka serikali kutekeleza mageuzi yanayolenga utoaji wa huduma jumuishi.

 Raila alisisitiza umuhimu wa kuweka maslahi ya taifa mbele ya tofauti za kisiasa, akihimiza njia ya pamoja katika uongozi wa nchi.

“Serikali lazima ijitahidi kwa njia endelevu kujifanya rafiki wa wananchi. Idadi ya vijana katika taifa letu inaongezeka kwa kasi, lakini huduma za umma zinaendelea kuzeeka.

“Mteja wa serikali siku hizi si tu kijana, bali pia ni msomi, mwenye ujasiri na akili. Amelelewa katika taifa lililo huru zaidi, la kidemokrasia na wazi. Kundi hili lenye msukosuko linahitaji serikali inayoweza kufikiwa kwa urahisi na haraka, isiyo na urasimu mwingi, na yenye ufanisi zaidi,” aliongeza.

Aliyasema hayo wakati wa warsha ya Tatu ya Baraza la Mawaziri iliyoandaliwa na Rais William Ruto katika eneo la Karen, Nairobi.

Rais William Ruto na Kiongozi wa ODM Raila Odinga

Warsha hiyo ndiyo ya kwanza tangu ODM na UDA kusaini makubaliano ya ushirikiano (MOU) yenye lengo la kuimarisha ajenda ya utoaji huduma kwa kuzingatia maslahi ya wananchi.

“Hii ndiyo warsha ya kwanza tangu ODM na UDA wasaini makubaliano ambayo si tu yaliokoa taifa bali pia yaliweka msingi wa ajenda pana ya kuunda mfumo wa utoaji huduma unaomlenga mwananchi, wenye ushirikishwaji, utendaji na uwazi,” alisema Odinga.

“Tathmini hii pia inafanyika wakati mgumu kwa nchi, ambapo wananchi wanatoa madai ya huduma bora na ushirikishwaji mkubwa katika uongozi. Hamasa hii pia inasababishwa na wale wanaohisi kuwa lazima wawe madarakani. Makundi yote haya ni raia wa Kenya. Wanastahili kusikilizwa.”

Aliongeza kuwa anatumaini kuwa tathmini ya sera na utendaji kazi wa serikali italeta uelewa na umiliki bora wa serikali na wananchi wake.

Raila alisisitiza haja ya serikali kushughulikia masuala ya wananchi na kuwashirikisha kikamilifu katika utungaji na utekelezaji wa sera.

Alisema kuwa mipango yote ya serikali inapaswa kuwa jumuishi, kuhakikisha kuwa hakuna eneo au kundi linabaki nyuma bila kujali matokeo ya uchaguzi.

“Ninaamini kwa dhati kwamba licha ya tofauti zetu, maono yetu au hata hali ya kukatishwa tamaa, lazima tuweke taifa mbele,” alisema.

Ruto, Raila na Waziri Wycliffe Oparanya

“Tunaweza kuwa na maono makubwa kadri tunavyotaka, lakini bila taifa la kuyatekeleza, yatabaki kuwa ndoto zisizotimizwa. Taifa lisilo kamili lakini linalojitahidi kuwa bora ni bora zaidi kuliko taifa lililoporomoka,” aliongeza.

Machafuko ya kijamii ya hivi karibuni yanaashiria hitaji pana la uongozi bora, jambo linalohitaji mipango ya serikali inayojibu mahitaji ya wananchi kwa uwazi.

Alitoa wito wa mabadiliko ndani ya mfumo wa serikali, akihimiza huduma ya umma yenye vijana wengi, inayofanya kazi kwa ufanisi na rafiki kwa wananchi ili kuwahudumia wananchi waliobobea kielimu.

Raila alionya dhidi ya mtazamo wa kudharau unaoonekana katika baadhi ya maafisa wa serikali, akisema kizazi cha sasa kinahitaji kuheshimiwa na njia rahisi ya kushiriki katika uongozi wa taifa.

Alisema kuwa utawala thabiti unahusiana moja kwa moja na kujenga taasisi imara za kitaifa, kuheshimu utawala wa sheria, na kupambana na ufisadi ili kudumisha imani ya wananchi kwa serikali.

Alisisitiza kuwa uwazi katika usimamizi wa fedha za umma na uwajibikaji kwa vitendo vya ufisadi ni muhimu katika kuimarisha tena imani ya wananchi kwa serikali.

Alitilia mkazo haja ya kuwepo kwa mfumo wa kuaminika wa kuripoti maendeleo halisi ya utawala kwa wananchi, ili kuimarisha hali ya umiliki na kuaminiana kati ya serikali na raia.

Ruto, Raila na mawaziri


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved