Mbunge wa Kapseret, Oscar Sudi, amewataka Wakenya, hasa kizazi cha Gen Z, kuacha kukabiliana kwa nguvu na maafisa wa polisi waliobeba silaha wakati wa maandamano. Sudi alisema tabia hiyo inavunja heshima na kudhalilisha maafisa hao.
Alisema maafisa wa polisi pia ni binadamu walioajiriwa kulinda Wakenya wote, na si sahihi kuwadharau hadharani na kupuuza kazi yao.
Mbunge huyo alilaani kifo cha hivi majuzi cha mwanablogu Albert Ojwang katika Kituo Kikuu cha Polisi, kilichosababisha hasira kwa umma, na kusema waliohusika lazima wawajibishwe.
Hata hivyo, alieleza kuwa mauaji hayo hayapaswi kutumiwa kama sababu ya waandamanaji kukabiliana na maafisa walioko kazini au kujaribu kuwanyang’anya silaha.
“Tunaomba vijana wetu waheshimu maafisa wetu kwa sababu wao pia ni watoto wetu, ndugu zetu na dada zetu. Tusiende mpaka kujaribu kuwanyang’anya bunduki,” alisema Sudi.
Alikuwa akizungumza katika eneo bunge la Kapseret ambako aligawa hundi za thamani ya Shilingi milioni 4.6 kwa makundi ya Uwezo.
Sudi alionya kuwa ukosefu wa nidhamu na heshima unaweza kusababisha machafuko, akisema haiwezekani nchi kuendelea bila maafisa wa usalama.
“Sote tunategemea maafisa hawa kwa ajili ya usalama wetu, na tunapaswa kushirikiana nao badala ya kuwageukia kwa sababu ya makosa ya watu wachache,” alisema.
Aliitaka Bunge kuimarisha sheria za kuwalinda maafisa wa polisi dhidi ya mashambulizi kutoka kwa raia wenye nia mbaya.
“Nilikuwako katika moja ya nchi jirani na walikuwa wakiniuliza kama tuna sheria nchini mwetu. Wanaona vurugu na ukosefu wa heshima uliopo kila mahali,” alisema Sudi.
Aliongeza kuwa jamii iliyostaarabika lazima itawaliwe na sheria pamoja na heshima ya pande zote.
Wakati huohuo, Sudi alikosoa wale wanaomshambulia Naibu Mkuu wa Polisi Eliud Lagat kabla ya uchunguzi kuhusu kifo cha Ojwang kukamilika.
Alisema kuwa ingawa Lagat ndiye aliyekuwa mlalamishi katika kesi iliyosababisha kukamatwa kwa Ojwang, hiyo haimaanishi moja kwa moja kwamba anahusika na kifo chake.
“Uchunguzi utatueleza ukweli, na kama Lagat atapatikana kuhusika, basi atapelekwa mahakamani,” alisema.
Sudi alidai kuwa wengi wa wanaotaka Lagat afutwe kazi wanafanya hivyo kwa chuki na visasi binafsi.
“Hatuhitaji kuchukiana au kuingiza siasa katika masuala ambayo tayari yameelezwa wazi kwenye sheria,” alisema.