
Viongozi wa Kenya Kwanza sasa wanadai kuwa kuna mpango wa upinzani kuwachochea vijana wa kizazi cha Gen Z kuandamana na kusababisha vurugu kote nchini.
Wakizungumza katika hafla tofauti zilizofanyika katika kaunti za Pokot Magharibi na Nyamira, viongozi hao walisema mpango huo unalenga kuvuruga miradi ya maendeleo ya serikali na kuleta mtafaruku usio wa lazima.
Walitahadharisha kuwa kampeni za kisiasa za mapema zinaongeza joto la kisiasa nchini kabla ya uchaguzi mkuu ujao.
“Mtu ana duka moja kidogo, ako hapo na stock yake ya elfu mia moja. Unaleta vurugu, vijana wanakuja wananyakua yote wanaenda nayo. Insurance hailipi,” Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula alsema.
“Wale wa siasa mfululizo, ukabila na chuki mfululizo, tuwaambiaje? Shindwe! Sisi tuendelee na kazi bila break? Kazi mfululizo? Maendeleo mfululizo?” alisema Kiongozi wa Wengi Bungeni Kimani Ichung’wah.
“Hakuna hata mtu mmoja atakayepoteza maisha kwa sababu yako. Ile taabu tungepata hapa next week, tunawaambia shetani ashindwe,” alisema Mbunge wa Mugirango Kusini Silvanus Osoro.
Kauli zao zinajiri wakati maandamano yaliyopangwa na kizazi cha Gen Z yanatarajiwa kufanyika tarehe 25 Juni 2025, kwa heshima ya waliopoteza maisha yao wakati wa maandamano ya mwaka jana kupinga Mswada wa Fedha.
Kamanda wa Polisi wa Nairobi George Seda alithibitisha kupokea mawasiliano rasmi kuhusu maandamano hayo yaliyopangwa na akasema kuwa Huduma ya Polisi itahakikisha usalama kwa wote.
“Wacha tuweke mipaka kwenye kile tunachokiita maandamano ya amani. Tusifanye maandamano yatakayowaathiri watu wengine ambao si sehemu ya waandamanaji,” alisema Seda siku ya Jumatano wiki hii.