
Uongozi wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM) umeitaka serikali kuendelea kuwafidia wanaopoteza maisha na wale waliojeruhiwa wakati wa maandamano.
Katibu Mkuu wa ODM, Edwin Sifuna, alisema katika taarifa siku ya Jumatatu kuwa msimamo wa chama haujabadilika.
“Msimamo wetu unabaki pale pale. Wala madai yetu kwamba ukatili wa polisi na utekaji wa raia lazima vikome hayajabadilika,” aliongeza.

Alisema waliingia katika ushirikiano na serikali ya Kenya Kwanza kwa ajili ya kudumisha taifa lenye amani.
Sifuna alisema kufanya kazi kwa karibu na serikali haina maana kwamba wanakubaliana na misimamo au sera za serikali ya Kenya Kwanza.
“Misingi yoyote ya uthabiti tunayokubaliana nayo kwa ajili ya kudumisha taifa lenye amani na demokrasia, haimaanishi kwamba tumejiunga na serikali,” aliongeza.
Aliitaka vyombo vya habari kuzingatia maadili ya uandishi wa habari kwa uwajibikaji, akibainisha kuwa hawatakubali kushinikizwa kufuata njia ya kutumikia maslahi binafsi.
“Kanuni ya uandishi wa habari ya ukweli, uaminifu na haki haiwezi kutolewa kafara kwa sababu ya kutafuta umaarufu wa kisiasa,” alisema Sifuna.
“Uongozi wa ODM na chama kwa ujumla unakataa kutishwa na kupotoshwa na propaganda za upendeleo zinazojificha kama uandishi wa habari,” aliongeza.
Sifuna alihimiza mshikamano wa kitaifa huku maandamano yaliyopangwa na kizazi cha Gen Z yakikaribia.
“Tunapokaribia kumbukumbu ya maandamano ya Gen Z, tunawahimiza Wakenya wenye nia njema kudumisha mshikamano wa kitaifa na kupuuza wale wanaotaka kutugawanya,” alisema Sifuna.
“Chama kwa muda mrefu kimekuwa mtetezi na mtekelezaji wa maandamano ya amani na mabadiliko, na tunawahimiza wote watakaoshiriki kuadhimisha kumbukumbu hiyo Jumatano hii kusimama bila woga upande wa uhuru na demokrasia, na haki ya kuandamana kama ilivyoainishwa katika katiba,” aliongeza.