logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Babake Mwanablogu Aliyeuawa, Albert Ojwang, Awasili Mahakamani Kibera Kusikiliza Kesi

Jaji Diana Mochache aliagiza washukiwa waendelee kuzuiliwa katika vituo walivyokuwa wakishikiliwa wakati wa uchunguzi.

image
na Tony Mballa

Habari24 June 2025 - 12:29

Muhtasari


  • Hii inajiri siku moja baada ya Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP) kuidhinisha mashtaka ya mauaji dhidi ya maafisa wa polisi watatu wanaohusishwa na mauaji ya mwanablogu huyo.
  • Maafisa hao ni Mkuu wa Kituo cha Polisi cha Nairobi Central, OCS Samson Talaam, pamoja na makonstebo James Mukhwana na Peter Kimani, ambao watashtakiwa pamoja na raia wengine watatu.

Baba wa Albert Ojwang, Meshack Opiyo, aliwasili katika Mahakama ya Kibera Jumanne kabla ya kuanza kwa kusikilizwa kwa kesi ya mauaji ya mwanawe.

Hii inajiri siku moja baada ya Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP) kuidhinisha mashtaka ya mauaji dhidi ya maafisa wa polisi watatu wanaohusishwa na mauaji ya mwanablogu huyo.

Maafisa hao ni Mkuu wa Kituo cha Polisi cha Nairobi Central, OCS Samson Talaam, pamoja na makonstebo James Mukhwana na Peter Kimani, ambao watashtakiwa pamoja na raia wengine watatu.

Albert Ojwang

Raia hao ni John Ngibe Gitau almaarufu Kinara, Gin Ammitou Abwao almaarufu Gilbeys, na Brian Mwaniki Njue, waliokuwa kizuizini katika kituo hicho cha polisi kabla ya kulipwa ili "kumfundisha adabu" marehemu, lakini waliishia kumuua katika harakati hizo.

"Taarifa kwa mshitakiwa kutoka kwa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) kwa niaba ya Jamhuri ni kwamba washukiwa waliotajwa hapo juu wameshtakiwa kwa kosa lifuatalo – mauaji kinyume na kifungu cha 203 kikisomwa pamoja na kifungu cha 204 cha Kanuni ya Adhabu," sehemu ya hati ya mashtaka inasomeka.

"Usiku wa tarehe 7 Juni 2025, kati ya saa 3:30 usiku na saa 8:00 alfajiri katika Kituo cha Polisi cha Central ndani ya jiji la Nairobi, kwa pamoja na wengine ambao hawapo mahakamani, walimuua Albert Omondi Ojwang," sehemu ya mashtaka inasema.

Jaji Diana Mochache aliagiza washukiwa waendelee kuzuiliwa katika vituo walivyokuwa wakishikiliwa wakati wa uchunguzi.

Meshack Opiyo

Washukiwa hao wanadaiwa kumuua marehemu akiwa mikononi mwa polisi baada ya kukamatwa na maafisa kutoka Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) nyumbani kwake Homa Bay.

Marehemu alikuwa amekamatwa na maafisa wa DCI kufuatia malalamiko yaliyowasilishwa na Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi, Eliud Lagat, kuhusu unyanyasaji wa kimtandao dhidi yake.

Makala Zinazohusiana


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved