logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Quickmart Yakanusha Madai Ya Miili Kupatikana Katika Tawi La OTC

Mashirika ya kutetea haki za binadamu likiwemo Amnesty International yaliweka idadi ya waliouawa kuwa 16.

image
na Tony Mballa

Habari26 June 2025 - 22:18

Muhtasari


  • Quickmart ilisisitiza kuwa usalama wa wafanyakazi wake, wateja na jamii kwa ujumla unasalia kuwa kipaumbele chake kikuu, na kwamba inachukua hatua stahiki kuhakikisha biashara inaendelea na imani ya umma inarejeshwa.
  • “Japokuwa tunatambua kuwa matukio ya hivi majuzi yameleta changamoto kubwa kwa matawi haya, tungependa kusisitiza kuwa Quickmart imejizatiti kurejesha hali ya kawaida kwa haraka iwezekanavyo,” kampuni hiyo ilisema.

Duka la jumla la Quickmart limekanusha madai yanayosambaa kwamba miili kadhaa ilipatikana ndani ya tawi lake la OTC jijini Nairobi kufuatia maandamano mabaya ya Jumatano.

Katika taarifa iliyotolewa Alhamisi, msururu huo wa rejareja ulikanusha vikali uvumi huo unaoenea mtandaoni, na kuwataka wananchi watulie huku ukisisitiza kuwa hakuna vifo wala majeruhi yaliyotokea katika matawi yake ya OTC au Ruiru, ambayo yote yaliathiriwa na machafuko hayo.

“Kinyume na taarifa potofu zinazosambaa kwenye majukwaa ya kidijitali, tungependa kuuhakikishia umma kwamba hakuna mfanyakazi, mteja au mtu mwingine yeyote aliyejeruhiwa au kufariki katika matawi hayo mawili,” ilisomeka taarifa hiyo.

Quickmart ilisisitiza kuwa usalama wa wafanyakazi wake, wateja na jamii kwa ujumla unasalia kuwa kipaumbele chake kikuu, na kwamba inachukua hatua stahiki kuhakikisha biashara inaendelea na imani ya umma inarejeshwa.

“Japokuwa tunatambua kuwa matukio ya hivi majuzi yameleta changamoto kubwa kwa matawi haya, tungependa kusisitiza kuwa Quickmart imejizatiti kurejesha hali ya kawaida kwa haraka iwezekanavyo,” kampuni hiyo ilisema.

Msururu huo wa maduka uliongeza kuwa unafanya kazi kwa bidii kuimarisha shughuli zake na kuwasaidia wanunuzi pamoja na wafanyakazi, huku ikiendelea kushirikiana na mamlaka na wadau husika.

“Quickmart inasalia kujali jamii yetu na itaendelea kuuarifu umma tunapojitahidi kuelekea kwenye uthabiti na urejeshwaji wa huduma.”

Wakati huohuo, Quickmart iliwashauri wateja wanaotumia matawi ya OTC na Ruiru yaliyoharibiwa, kufika katika matawi mengine yaliyo karibu ili kuendelea kupata huduma bila usumbufu.

Ufafanuzi huu umetolewa kufuatia machafuko makubwa yaliyozuka katika kaunti mbalimbali siku ya Jumatano, wakati maelfu ya watu walimiminika mitaani kuadhimisha mwaka mmoja tangu maandamano ya kupinga Mswada wa Fedha yaliyoongozwa na kizazi cha Gen Z.

Waziri wa Usalama wa Ndani Kipchumba Murkomen alithibitisha katika mkutano na wanahabari kuwa angalau watu 10 waliuawa, ingawa alibainisha kuwa uchunguzi kuhusu mazingira na idadi kamili ya vifo bado unaendelea.

Mashirika ya kutetea haki za binadamu likiwemo Amnesty International yaliweka idadi ya waliouawa kuwa 16.

Murkomen pia aliripoti kuwa maandamano hayo yalisababisha uharibifu mkubwa wa mali ya serikali na ya umma, ikiwa ni pamoja na mashambulizi dhidi ya vituo vya polisi na miundombinu muhimu.

Miundombinu kama barabara, reli, laini za umeme na vifaa vya maji pia viliharibiwa, hali ambayo Murkomen aliielezea kama “shambulio lililopangwa na kuchochewa kisiasa dhidi ya uthabiti wa taifa.”

Makala Zinazohusiana


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved