
Watu wasiopungua 19 walipoteza maisha yao wakati wa maandamano ya kizazi cha Gen Z yaliyogeuka kuwa machafuko siku ya Jumatano.
Ripoti ya Tume ya Kitaifa ya Haki za Binadamu ya Kenya (KNCHR) pia ilibaini kuwa watu 531 walijeruhiwa kwa njia mbalimbali.
KNCHR ilisisitiza kuwa kulikuwa na visa 15 vya watu kutoweka kwa kulazimishwa, na kuongeza kuwa watu 179 walikamatwa. Wanawake watatu waliripotiwa kubakwa, mmoja wao na kundi la watu. Kulikuwa pia na kesi 2 za ubakaji wa mtu mmoja mmoja.
“Tume inalaani vikali ukiukaji wote wa haki za binadamu na inasisitiza uwajibikaji kutoka kwa wahusika wote. Tunatoa tena rambirambi zetu kwa wale waliopoteza wapendwa wao na tunawatakia ahueni ya haraka walioumia,” ilisoma taarifa ya KNCHR.