
Waziri wa Usalama wa Ndani Kipchumba Murkomen amesisitiza kuwa agizo lake kwa maafisa wa usalama kuwapiga risasi watu wanaokaribia vituo vya polisi linalindwa na Katiba.
Waziri huyo amekosolewa vikali, huku Wakenya kutoka sekta mbalimbali wakitafsiri matamshi yake kuwa ni ruhusa kwa maafisa wa usalama kutekeleza mauaji ya kiholela dhidi ya raia.
Alhamisi, Juni 26, muda mfupi baada ya kuhutubia wanahabari kuhusu hali ya nchi kufuatia maandamano ya Gen Z—ambayo aliyataja kuwa jaribio la mapinduzi—Murkomen aliagiza polisi kuwachukulia hatua kali wote watakaojaribu kuingia katika vituo vya polisi.
"Na tumeambia polisi, mtu yeyote atakaribia police station, piga yeye risasi," alisema Murkomen.
Katika taarifa aliyotoa Jumamosi, Waziri huyo alifafanua kuwa matamshi yake yalitolewa kwa kuzingatia masharti ya kisheria.
Alinukuu Ratiba ya Sita ya Sheria ya Huduma ya Polisi ya Kitaifa, inayoweka masharti ya ni lini afisa wa polisi anaweza kutumia silaha, ikiwa ni pamoja na kulinda maisha, mali, au kwa kujihami.
"Kauli yangu ilitolewa kwa muktadha na kwa utambuzi kamili, nikiwa na ufahamu wa wazi wa masharti ya sheria. Hakuna kiongozi, msomi, mwanasheria, mwanahabari, mwanablogu, au mtoa maoni ambaye amenipinga kwa misingi ya kisheria," alisema Murkomen.
"Kwa umri, nafasi na uzoefu nilio nao, siwezi kutoa matamshi ambayo hayana msingi wa kikatiba na kisheria. Katika taaluma yangu yote, sijawahi kuwa upande wa makosa ya kisheria kwa sababu ya matamshi au matendo yangu."
Waziri huyo pia alibainisha kuwa hana mamlaka ya kumuagiza Inspekta Jenerali wa Polisi au Huduma ya Polisi ya Kitaifa kufanya jambo lolote nje ya mipaka ya sheria.
"Nawaomba wale wanaoeneza taarifa potofu, za upotoshaji, na habari za uongo wanipinge kwa misingi ya sheria. Wanaodai kuwa nilitoa amri kwa polisi waonyeshe hiyo amri iko wapi. Kusema tu yale yaliyo katika sheria si sawa na kutoa amri kwa polisi," alisema Murkomen.
"Polisi wanalazimika kufanya kazi kwa mujibu wa Katiba, sheria husika, na maagizo ya ndani ya idara. Kwa vyovyote vile, sina mamlaka ya kikatiba ya kutoa amri kama hizo; jukumu langu ni kuwaunga mkono polisi na kutoa mapendekezo ya sera yatakayosaidia utekelezaji wa sheria na kudumisha utulivu."
Alisisitiza kuwa maafisa wa polisi wamepewa mamlaka ya kikatiba ya kujilinda dhidi ya waandamanaji wanaohatarisha maisha yao.
"Maafisa wetu wa polisi wanaoshambuliwa na majambazi, waandamanaji, na wateketezaji—walioteketeza vituo vya polisi, kuiba bunduki, kuwachoma washukiwa wakiwa hai, na kuharibu mali ya mamilioni ya shilingi, ikiwemo majengo ya mahakama—hawawezi kuachwa bila msaada ilhali wamepewa mamlaka ya kikatiba na kisheria ya kujilinda, kuwalinda raia na mali yao."
Agizo la Murkomen la "piga risasi kuua" lilikumbwa na upinzani mkali kutoka kwa Chama cha Wanasheria wa Kenya (LSK), ambacho kililitaja kuwa ni matamshi ya kiholela na kuonya kuwa yanaweza kuchochea mauaji ya kiholela.