
Kiongozi wa chama cha People's Liberation Party (PLP), Martha Karua, amemtaka Rais William Ruto aheshimu sauti ya wananchi na kujiuzulu mara moja.
Katika mahojiano na kituo kimoja cha redio cha humu nchini, Karua alitaka Ruto pamoja na serikali yake yote kung'atuka mamlakani.
Kauli yake inajiri wakati ambapo hasira zinaendelea kupanda miongoni mwa Wakenya wanaolalamikia uongozi wa Ruto kwa kushamiri kwa ufisadi, kupuuzwa kwa mahitaji ya wananchi wa kawaida, kupanda kwa gharama ya maisha, ukatili wa polisi, mauaji ya kiholela, na kukamatwa kiholela kwa wakosoaji wa serikali.
Karua alimkumbusha Ruto kuwa Wakenya wana chaguo la kumuondoa madarakani hata kabla ya muhula wake kukamilika, iwapo hatachagua kuondoka kwa hiari.
“Pitia njia ile ile uliyopita kufika hapo. Unaweza kujiuzulu; kama ungekuwa unaiheshimu kweli sauti ya wananchi, ungekuwa umejiuzulu tangu sasa, pamoja na serikali yako yote, na mrudi nyumbani,” waziri huyo wa zamani wa sheria alisema katika mahojiano na Spice FM siku ya Jumanne.
“Lakini kwa sababu hutaki, iwe ni 2027 au hata kabla ya hapo, wananchi watakuondoa. Unaweza kuendelea kuua kama unavyofanya sasa, lakini huwezi kuua kila mtu,” aliongeza, akirejelea visa vinavyozidi kuongezeka vya polisi kuwaua waandamanaji wanaopinga serikali.
Akimlinganisha Ruto na Idi Amin Dada, dikteta wa kijeshi wa Uganda aliyeondolewa madarakani mwaka 1979, Karua alisema hatavuka kile anachokiita “mapenzi ya wananchi.”
“Historia imetuonyesha watawala wa mabavu waliotawala kwa hofu, na hakuna hata mmoja wao aliyewahi kushinda mapenzi ya wananchi,” alisema.
“Siyo hata Idi Amin, ambaye Ruto anaonekana kumwiga. Bashir alikuwa na jeshi lenye nguvu sana lakini bado aliangushwa.”
Kwa mujibu wa kiongozi huyo wa PLP, “nguvu iko kwa wananchi,” na Wakenya wanaweza “kufukuza” Ruto kwa kile anachokiita serikali iliyopindua Katiba.
“Wakenya wana haki ya kukuondoa kwa kushindwa kabisa kuongoza, kwa kukiuka utawala wa sheria, na kwa kujaribu kupindua Katiba. Sheria inasema huwezi kuunda serikali isipokuwa kwa njia halali, lakini Ruto amepindua Katiba na kuanzisha utawala dhalimu,” Karua alisema.
“Ikiwa kweli anajiheshimu na anawaheshimu wananchi, anapaswa kuanza kufunga mizigo.”
Anamtuhumu Ruto kwa kubeza vuguvugu la vijana na kuwatunga wananchi wenye sauti na wanaharakati wa haki za binadamu makosa ya vurugu za maandamano zinazodaiwa kusababishwa na mawakala wa serikali.
Karua alimkosoa Ruto kuhusu hatua ya serikali kufunga kwa uzio maeneo muhimu kama Bunge na Ikulu kabla ya maandamano ya Jumatano iliyopita yaliyokuwa ya kuwaenzi waliouawa katika maandamano dhidi ya mswada wa fedha mwaka jana.
“Uoga wa Dkt. William Ruto ni wa kihistoria. Mimi niko mwishoni mwa miaka ya 60, na sijawahi kuona rais anayejifungia nyuma ya nyaya za miiba.
Ikulu si mali yako binafsi, Bw. Ruto. Ni nyumba ya wananchi. Ukifunga nyumba yako binafsi kule Sugoi au Karen, hakuna atakayekuuliza. Lakini kama Ikulu ni moto kwako, kwa nini usiende likizo Karen? Waachie wananchi waingie katika nyumba yao,” Karua alisema.
Rais, siku ya Ijumaa, alipuuzilia mbali kelele za Wakenya waliokwisha mtaja kama rais wa muhula mmoja, wakisema hatarudi madarakani mwaka 2027.
“Ikiwa ni suala la mihula, Katiba imeshaliweka hilo bayana. Unaweza kuwa wa muhula mmoja au miwili… huwezi kuwa na zaidi ya hapo. Hii mbwembwe yote kuhusu mihula ni ya nini?” Ruto alihoji.
“Ikiwa ni Ruto lazima aondoke, basi niambie mnataka niondoke vipi. Unamaanisha nini unaposema Ruto lazima aondoke? Niondoke vipi? Kwa sababu tunayo Katiba.”