logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Chama cha Kisiasa cha Eugene Wamalwa Chamkosoa Ruto kwa Kujenga Kanisa la Shilingi Bilioni 1.2 Ikulu

Ukosoaji wa DAP-K unaonyesha hasira inayozidi kuongezeka miongoni mwa wananchi, wengi wakihisi kuwa serikali inapuuza sekta muhimu.

image
na Tony Mballa

Habari04 July 2025 - 11:45

Muhtasari


  • Mnamo Juni 19, 2025, Bunge liliidhinisha Mswada wa Fedha ili kufadhili bajeti ya Shilingi trilioni 4.29.
  • Mswada huo ulisainiwa kuwa sheria na Rais William Ruto mnamo Juni 26, ukibainisha kuwa Shilingi bilioni 1,805.02 zitatumika kwa matumizi ya kawaida huku Shilingi bilioni 744.52 zikielekezwa kwa miradi ya maendeleo.

Chama cha Democratic Action Party of Kenya (DAP-K) kimetoa lawama kali dhidi ya serikali kuhusu kile ilichokitaja kuwa ni mgao wa Shilingi bilioni 1.2 kwa ajili ya kujenga kanisa jipya katika Ikulu, kikieleza kuwa huo ni upendeleo usiofaa.

Kupitia chapisho lililotumwa kwenye mtandao wa X mnamo Julai 4, 2025, chama hicho kilielezea hali mbaya ya shule, hospitali na miundombinu mingine muhimu, kikituhumu serikali kwa kupuuza mahitaji ya umma.

“Wakati shule, hospitali na miundombinu mingine ya lazima ikiendelea kusalia katika hali mbaya, Kaongo anajenga kanisa la Ksh 1.2B Ikulu. Vipaumbele kama hivi ndivyo vinavyowafanya Wakenya kusimama kidete…. Huzuni kubwa sana!” ilisoma taarifa ya DAP-K.

Eugene Wamalwa

Kanisa hilo, ambalo linadaiwa kujengwa kwa ajili ya ibada ndani ya viunga vya Ikulu, limeibua mjadala mpana kote nchini.

Ukosoaji wa DAP-K unaonyesha hasira inayozidi kuongezeka miongoni mwa wananchi, wengi wakihisi kuwa serikali inapuuza sekta muhimu.

Shule nyingi nchini hukosa madarasa bora, vitabu na walimu wa kutosha, huku hospitali za umma zikikumbwa na ukosefu wa vifaa vya kisasa na upungufu wa dawa.

Miundombinu kama barabara pia imeendelea kuwa katika hali mbaya, jambo linaloathiri maisha ya kila siku na ukuaji wa uchumi.

Eugene Wamalwa

Wakosoaji wanasema kuwa serikali inapaswa kuelekeza rasilimali zake kurekebisha miundombinu inayoporomoka na kuboresha huduma za umma badala ya kufadhili mradi wa kifahari kama ujenzi wa kanisa la Ikulu.

Mnamo Juni 19, 2025, Bunge liliidhinisha Mswada wa Fedha ili kufadhili bajeti ya Shilingi trilioni 4.29.

Mswada huo ulisainiwa kuwa sheria na Rais William Ruto mnamo Juni 26, ukibainisha kuwa Shilingi bilioni 1,805.02 zitatumika kwa matumizi ya kawaida huku Shilingi bilioni 744.52 zikielekezwa kwa miradi ya maendeleo.

Eugene Wamalwa

Mswada huo pia ulijumuisha hatua za kupunguza ushuru, kama vile kuondoa makato kwenye marupurupu ya kustaafu na kuongeza kiwango kisichotozwa ushuru kwa posho za safari kutoka Shilingi 2,000 hadi Shilingi 10,000.

Hata hivyo, ulizua maandamano kutokana na hofu kuwa ungezidisha gharama ya maisha, huku wakosoaji wakisema ungewaumiza Wakenya wa kawaida.

Hadi sasa, hakuna taarifa rasmi kama mgao wa Shilingi bilioni 1.2 kwa ajili ya kanisa umetolewa kutoka bajeti ya mwaka wa fedha 2025/2026, bajeti ambayo tayari imezua mjadala mkubwa kufuatia kupitishwa kwa Mswada wa Fedha wa 2025.

Makala Zinazohusiana


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved