
Aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua amemshambulia Rais William Ruto, akidai kuwa kiongozi huyo wa taifa anatekeleza mpango wa kutesa jamii ya Mlima Kenya kwa njia ya kimfumo.
Aliyanena hayo Jumamosi wakati wa mazishi ya shangazi yake, marehemu Gladys Gathoni Kahua, katika Kaunti ya Nyeri.
Gachagua alieleza majuto makubwa kwa kupuuza onyo la awali kutoka kwa shangazi yake kuhusu nia ya kisiasa ya Ruto.
“Kama ningemsikiliza shangazi yangu, tusingekuwa katika hali hii,” alisema Gachagua. “Alinionya kuwa Ruto angenianza mimi, kisha watoto wangu, na hatimaye jamii yangu. Sikuamini wakati huo. Lakini leo, yote yanatimia kama alivyosema.”
Gachagua alimtuhumu Rais Ruto kwa kupanga msako wa kisiasa katika taasisi muhimu za serikali kwa kuwaondoa kimakusudi watu kutoka eneo la Mlima Kenya kwenye nyadhifa za juu serikalini.
Aidha, alidai kuwa agizo la siri lilitolewa Jumamosi iliyopita katika Ikulu ya Nairobi, ambapo Ruto anadaiwa kukutana na makamanda wa polisi wa mikoa na kuwaagiza kulenga wanajamii wa eneo hilo.
“Shida yetu kubwa ni uamuzi uliotolewa Jumamosi iliyopita katika Ikulu, ambapo aliwaita makamanda wote wa polisi na kuwaagiza waanzishe msako na mateso dhidi ya jamii yetu, na tayari umeanza kwa kasi. Kati ya watu zaidi ya 400 waliokamatwa, asilimia 92 ni kutoka jamii hii... kwa tuhuma zilizotungwa,” Gachagua alidai.
Aliendelea kumtaja Mbunge wa Kikuyu Kimani Ichung’wah, akimtuhumu kushirikiana na Rais kunyamazisha wapinzani na kutisha waandamanaji vijana.
Gachagua alidai kuwa Ichung’wah ndiye aliyesukuma kukamatwa kwa kiongozi wa vijana wa chama cha Democracy for the Citizens Party (DCP) katika Kaunti ya Kiambu, Peter Kinyanjui maarufu kama Kawanjiru, akimtuhumu kushiriki katika kuchoma mahakama ya Kikuyu na kuvamia kituo cha polisi cha Dagoretti.
Gachagua pia alieleza majuto yake na kuwaomba radhi watu wa Mlima Kenya kwa kuunga mkono azma ya urais ya Ruto mwaka 2022.
“Nataka mnisamehe. Hali hii mbaya tuliyo nayo kama jamii ni kosa langu kwa sababu sikumsikiliza shangazi yangu. Kama jamii, tuko matatani na tuko njia panda. Shangazi yangu alinionya kuwa William Ruto ni mtu mwovu,” alisema Gachagua.