
Waziri wa Usalama wa Ndani Kipchumba Murkomen amewahimiza Wakenya kudumisha amani kabla ya maandamano yaliyopangwa ya Saba Saba.
Murkomen alisema kuwa maafisa wa polisi hawapaswi kulaumiwa kwa kushughulikia hali zinazotishia usalama wa umma wakati wa maandamano.
Aliahidi kuhakikisha kuwa watu wanaosababisha fujo wakati wa maandamano wanachukuliwa hatua za kisheria.
Waziri huyo aliwataka polisi waendelee kuwa na urafiki kwa wananchi, lakini wachukue hatua kali dhidi ya wahuni wanaotumia maandamano kama kisingizio cha kuharibu mali.
“Polisi wanapaswa kuchukua hatua dhidi ya wahuni na waandamanaji wanaonuia kusababisha vurugu wakati wa maandamano,” alisema.
Akizungumza Jumapili wakati wa harambee ya kuchangisha fedha kwa ajili ya Kanisa Katoliki katika eneobunge la Tigania Magharibi, kaunti ya Meru, Murkomen alitangaza kuwa Tigania Magharibi itagawanywa na kuwa kaunti ndogo mbili zaidi.
Akizungumzia suala la usalama katika mpaka wa Tigania, Igembe na Isiolo, waziri huyo alisema kuwa wizara yake inafanya kazi kwa bidii kutokomeza ukosefu wa usalama na uhalifu wa kutumia silaha katika maeneo hayo ya mpakani.
Aliwapongeza maafisa wa polisi kwa kazi yao nzuri na kujitolea kwao kulihudumia taifa.
Murkomen pia aliwahimiza wafugaji kushirikiana kwa karibu na polisi ili kukomesha wizi wa mifugo.
Mbunge wa Tigania Magharibi John Mutunga alidai kuwa viongozi wa upinzani ni wapiga kelele tu wasiokuwa na ajenda yoyote ya maana kwa taifa.
Aliwataka wakazi wa Meru kumuunga mkono rais kwa ajili ya maendeleo ya eneo hilo.