logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Raila Aeleza Sababu ya Kukosa Maadhimisho ya Saba Saba Kamukunji

Raila alitumia fursa hiyo kukumbuka historia ya kisiasa ya Kenya, akieleza harakati za kupigania mfumo wa vyama vingi.

image
na Tony Mballa

Habari07 July 2025 - 17:09

Muhtasari


  • Raila pia alieleza jinsi alivyosaidia kuandaa mkutano kati ya Matiba, Rubia na Jaramogi Oginga Odinga ili kuimarisha juhudi hizo za kutetea demokrasia.
  • Alifafanua kuhusu ukamataji na kifungo kilichofuata, ikiwa ni pamoja na yeye mwenyewe kukamatwa tarehe 4 Julai 1990 pamoja na wanaharakati wengine kama Gitobu Imanyara na John Khaminwa.

Aliyekuwa  Waziri MKuu Raila Odinga, ameeleza sababu ya kutohudhuria maadhimisho ya Siku ya Saba Saba katika uwanja wa Kamukunji jijini Nairobi, akisema alikumbana na vizuizi vya barabarani vilivyosambaa kote jijini vilivyomzuia kufika kwenye hafla hiyo.

“Nilikusudia kwenda Kamukunji kuungana na Wakenya wengine kuadhimisha siku hii muhimu sana. Kwa bahati mbaya, kama mnavyojua hali ya leo, kulikuwa na vizuizi vya barabarani kila mahali jijini, hali iliyowafanya watu washindwe kufika Kamukunji,” alisema Raila.

Raila alitumia fursa hiyo kukumbuka historia ya kisiasa ya Kenya, akieleza harakati za kupigania mfumo wa vyama vingi.

Alisema kuwa mnamo mwaka wa 1982, serikali ilibadilisha katiba na kuifanya Kenya kuwa taifa la chama kimoja pekee.

Aliangazia mchango wa viongozi wakuu kama vile Kenneth Matiba na Charles Rubia, ambao mwaka wa 1990 walitoa wito kwa umma wa kutaka mfumo wa vyama vingi na baadaye wakakamatwa.

“Mwaka 1982, wakati baadhi yetu tulitaka kuanzisha chama cha siasa, utawala wa wakati huo ulipeleka mswada bungeni na kuanzisha kifungu cha 2A kilichofanya kuwa kinyume cha sheria kuunda chama kingine cha siasa,” alisema.

“Mwaka 1990, wakati huo nilikuwa tayari nimekamatwa na kufungwa mara mbili. Kenneth Matiba na Charles Rubia tarehe 2 Mei 1990 waliitisha mkutano na waandishi wa habari na kusema kuwa wakati umefika kwa Kenya kuwa nchi ya vyama vingi, kwamba Wakenya wanataka mfumo wa vyama vingi.”

“Walilaaniwa vikali kama wanasiasa wa kikabila, wapinga utawala, na watu waliotaka kuleta vurugu nchini,” alisema.

“Kenneth Matiba alinifuata ili nipange mkutano kati yake na Jaramogi Oginga Odinga. Nilipanga mkutano huo, walikutana na Rubia, Oneko na baada ya majadiliano wakaamua kuwa wangewasaidia. Mwaka huo huo wa 1990, Matiba na Rubia walikamatwa na kuwekwa kizuizini,” alisema.

Raila pia alieleza jinsi alivyosaidia kuandaa mkutano kati ya Matiba, Rubia na Jaramogi Oginga Odinga ili kuimarisha juhudi hizo za kutetea demokrasia.

Alifafanua kuhusu ukamataji na kifungo kilichofuata, ikiwa ni pamoja na yeye mwenyewe kukamatwa tarehe 4 Julai 1990 pamoja na wanaharakati wengine kama Gitobu Imanyara na John Khaminwa.

Alieleza kuwa Rubia alipata matatizo makubwa ya kiafya akiwa kizuizini yaliyosababisha apoteze uwezo wa kuzungumza.

“Tarehe 4 Julai, nilikamatwa na kuwekwa kizuizini. Usiku huo huo, walimkamata Gitobu Imanyara na John Khaminwa. Paul Muite alienda mafichoni. Tume ya Kimataifa ya Wanasheria ilijitokeza na kuanzisha kampeni kubwa ya kuachiliwa kwa Khaminwa na Imanyara. Sisi wengine tulibaki kizuizini. Rubia ndiye aliyepatwa kwanza; alipata maambukizi mabaya sana, alipelekwa hospitalini, hatimaye alipoteza sauti na akaachiliwa,” alisema.

Makala Zinazohusiana


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved