
Msichana mwenye umri wa miaka 12 kutoka Kiambu, Bridget Njoki Wainaina, amefariki dunia baada ya kudaiwa kupigwa risasi na polisi alipokuwa akitazama runinga nyumbani siku ya Jumatatu.
Bridget alikosa kuhudhuria shule kutokana na hali ya taharuki iliyokuwepo kuhusiana na maandamano ya Saba Saba.
Akielezea tukio hilo, mama yake alisema walisikia mlio mkubwa na walipomuangalia Bridget, walimkuta akiwa amejeruhiwa kichwani.
"Ilipofika saa 12:20 jioni, tulisikia mlio mkubwa. Nilipomtazama binti yangu, niliona damu mikononi mwake.
"Mwanzoni nilidhani alikuwa amekwaruzwa, lakini nilipotazama kwa makini, niliona tundu kichwani. Hapo ndipo nilipopiga kelele kuomba msaada, na baba yake akaingia," mama huyo alieleza.
Licha ya juhudi za madaktari katika Hospitali ya St. Bridget kumuokoa, hawakuweza kumfufua.
"Tulimkimbiza katika Hospitali ya St. Bridget, ambapo madaktari walijaribu kumrudishia fahamu na kumwandaa kwa upasuaji. Waligundua kuwa moyo wake ulikuwa umesimama.
"Baada ya majaribio mengi bila mafanikio ya kumfufua, madaktari walilazimika kutangaza kuwa amefariki dunia," alisema.
Mama wa msichana huyo alielezea huzuni ya kina, akisema amempoteza binti mchapakazi na mwenye ndoto kubwa.
Tukio hilo limezua hasira kubwa miongoni mwa wananchi na viongozi, likielekeza tena macho kwenye wasiwasi unaoendelea kuhusu ukatili wa polisi nchini Kenya.
Mbunge wa Githunguri, Gathoni Wamuchomba, alikosoa agizo la "piga na uue" lililotolewa na Waziri wa Usalama wa Ndani, Kipchumba Murkomen, akipinga uhalali wa kumuua mtoto asiye na hatia.
"Nina uchungu na moyo wangu umevunjika kuona vijana wengi wakifariki kwa kupigwa risasi wakati wa maandamano.
"Tunaweza kuthibitisha kuwa agizo la hivi majuzi la Waziri wa Usalama la kupiga na kuua lilichukuliwa kwa uzito. Lakini kwa nini upige risasi hadi afe msichana asiye na hatia?" Wamuchomba aliandika.
Tukio hili ni sehemu ya mfululizo wa matukio ya kusikitisha, kama ilivyoonekana kwenye kisa cha awali cha mtoto mwingine, Kennedy Onyango, aliyepigwa risasi mara kadhaa wakati wa maandamano ya awali.
Kennedy pia alikuwa mwathiriwa mchanga wa ukatili wa polisi, alipigwa risasi mara kadhaa alipokuwa nje wakati wa machafuko.