
Boniface Kariuki, mchuuzi aliyepigwa risasi kichwani na polisi wakati wa maandamano katikati mwa jiji la Nairobi mnamo Juni 17, 2025, amezikwa leo Ijumaa katika eneo la Kangema, Kaunti ya Murang’a.
Kariuki alipigwa risasi kwa karibu na kukimbizwa katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta, ambako alifanyiwa upasuaji. Alilazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi kwa wiki mbili kabla ya kutangazwa kuwa ubongo wake haukuwa tena na uhai.
Uchunguzi wa maiti ulionyesha kuwa alifariki kutokana na jeraha kubwa kichwani. Vipande vinne vya risasi vilipatikana vikiwa vimekwama kwenye ubongo wake.
Wakati wa ibada ya wafu iliyofanyika Jumatano katika Kanisa Kuu la Holy Family Basilica jijini Nairobi, waombolezaji walimtaja Kariuki kuwa Mkenya mtiifu wa sheria na mchapakazi.
Mazishi yake imefanyika siku moja baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) kuidhinisha mashtaka ya mauaji dhidi ya Konstebo wa Polisi Klinzy Masinde Barasa kuhusiana na tukio hilo la kupigwa risasi lililosababisha kifo chake.
“Baada ya kukamilika kwa uchunguzi na kukusanywa kwa ushahidi, Baraza sasa atafunguliwa rasmi mashtaka ya mauaji dhidi ya mchuuzi huyo wa barakoa,” DPP alieleza.
Hata hivyo, mshukiwa mwenzake, Duncan Kiprono, ambaye alionekana pamoja naye katika tukio hilo lililonaswa kwenye kamera, ameachiwa huru.
Video za tukio hilo, zilionyesha afisa wa polisi anayeaminika kuwa Baraza akiwakimbilia waandamanaji kwenye Barabara ya Mondlane karibu na Imenti House kabla ya kufyatua risasi ya kwanza.
Picha hizo zilimwonyesha Kariuki akiwa amelala chini akivuja damu, huku waandamanaji waliokuwa wamechanganyikiwa wakimkimbilia kutoa msaada. Alikimbizwa katika Kituo cha Matibabu cha Bliss, ambako alipokea huduma ya kwanza ya dharura walipokuwa wakingoja gari la wagonjwa.
Baadaye alihamishiwa Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta jijini Nairobi, ambako juhudi za kuokoa maisha yake hazikufaulu.
Kariuki, aliyekuwa katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) katika KNH, alifariki dunia saa 9:15 alasiri Jumatatu, Juni 30, takriban wiki mbili baada ya tukio hilo.
Kifo chake kilizua hasira kubwa miongoni mwa watetezi wa haki za binadamu na umma kwa jumla, si tu kwa sababu hakuwa na silaha, bali pia kwa sababu maandamano hayo yalikuwa yakipinga ukatili wa polisi – ukatili ambao hatimaye ulimgharimu maisha yake.
Baraza na mshukiwa mwenzake (ambaye sasa ameondolewa mashtaka) walikamatwa muda mfupi baada ya tukio hilo, na mnamo Juni 19 walifikishwa katika Mahakama ya Milimani, ambapo jaji alikubali ombi la upande wa mashtaka na utetezi kuwashikilia kwa siku 15 ili kuruhusu uchunguzi zaidi kufanywa na Mamlaka Huru ya Uangalizi wa Polisi (IPOA).
Maafisa hao wawili walikuwa wakihudumu katika Kituo cha Polisi cha Kileleshwa, Nairobi, na walikuwa wametumwa kushika doria wakati wa vurugu zilizoshuhudiwa wakati wa tukio hilo.
Wakati huo huo, mazishi ya Kariuki yanaendelea leo nyumbani kwao Kangema, Kaunti ya Murang’a, kufuatia ibada ya wafu iliyofanyika Jumatano katika Kanisa la Holy Family Basilica jijini Nairobi.