
Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga amemkosoa vikali Naibu Rais wa zamani Rigathi Gachagua, ambaye pia ni kiongozi wa chama cha DCP, kwa kujaribu kugawanya nchi alipokuwa katika wadhifa wa juu serikalini.
Raila alimlaumu Gachagua kwa madai yake kuwa baadhi ya makabila hayakuwa na hisa (shares) serikalini kwa sababu hayakuunga mkono serikali ya Rais William Ruto katika uchaguzi wa Agosti 2022.
"Kenya ni ya Wakenya wote, iwe ni Mluo, Mkikuyu, Msomali, Mkalenjin, Mmijikenda au Mmaasai. Hakuna mtu anayemiliki nchi hii. Ni lazima tuijenge pamoja au tuione ikisambaratika," alisema Raila.
Odinga pia alikataa vikali kauli ya “Ruto must go” akisema kuwa kubadilisha tu rais hakutatatua matatizo ya taifa.
Akizungumza katika ibada ya mazishi huko Bomet siku ya Jumamosi, kiongozi huyo wa ODM alisisitiza haja ya uwakilishi jumuishi wa vizazi mbalimbali, akipendekeza wajumbe 40 kutoka kila kaunti 47.
"Hili halipaswi kuwa la kizazi kimoja tu, lazima liwakilishe utofauti kamili wa Wakenya," alisema.
Kwa mujibu wa Raila, asilimia 50 ya wajumbe hao wanapaswa kuwa vijana huku asilimia iliyosalia ikijumuisha watu wa makamo na wazee kutoka sekta mbalimbali.
"Nimependekeza kila kaunti itume watu 40—20 wawe vijana na wengine 20 wawakilishe wazee, wanawake, watu wenye ulemavu, wakulima, wafanyabiashara na wanaharakati wa kijamii," alisema.
"Na nimependekeza ya kwamba tuanze hii mazungumzo mwezi ujao."
Alisisitiza kuwa ni kupitia mazungumzo ya kina ya aina hiyo pekee ndipo mgogoro wa kisiasa na kijamii wa nchi unaweza kutatuliwa.
Kwa mujibu wa Raila, maandamano yanayoendelea ambayo alisema yanaongozwa na vijana, yanasababishwa na hali halisi ya kukatishwa tamaa ambayo ni lazima kusikilizwa na siyo kukandamizwa.
"Vijana hawa hawaandamani tu kwa sababu ya kuandamana. Hao ni watoto wetu. Ni lazima tuwasikilize na tuzungumze nao," aliongeza.
Alionya kuwa kushindwa kushughulikia hasira za umma kunaweza kuwa na athari kubwa.
"Hatutaki kuelekea uchaguzi wa 2027 tukiwa na chuki zaidi. Hasira ni hasara," alisema.
Raila pia alikataa vikali wazo la ‘Ruto lazima aende,’ akisema kwamba hata akibadilishwa, hali haitabadilika ikiwa mizizi ya matatizo haitashughulikiwa.
"‘Ruto lazima aende’ si suluhisho. Hata ukiweka Gachagua pale, hakuna kitakachobadilika kama hatutashughulikia chanzo cha matatizo," alisisitiza.
Raila alitoa pendekezo la mkutano huu kwa mara ya kwanza wiki iliyopita wakati wa maadhimisho ya siku ya Saba Saba, akisema mkutano huo utakuwa na jukumu la kuunda “mageuzi yasiyoweza kubatilishwa” ili kushughulikia ukatili wa polisi, ukosefu wa ufanisi wa mahakama, ufisadi na ukosefu wa ajira kwa vijana.
Alipendekeza matokeo ya mkutano huo yapelekwe kwa kura ya maoni ya umma ili kuimarisha mamlaka ya wananchi katika mwelekeo wa taifa.
Baadhi ya wabunge wamepinga pendekezo hilo, wakisema kuwa mabadiliko yanapaswa kuletwa na kura na si mazungumzo.
Gachagua: Jamii ya Wakikuyu Yajutia Kutomsikiliza Uhuru Kuhusu Ruto
Naibu Rais wa zamani Rigathi Gachagua alitaja pendekezo hilo la mkutano kuwa mbinu ya kukwepa uwajibikaji wa uchaguzi, na kuwataka raia kujiandaa kwa ushiriki wa maana kwenye uchaguzi wa 2027.