
Kiongozi wa chama cha DCP Rigathi Gachagua amemshambulia vikali waziri mkuu wa zamani Raila Odinga, akidai kuwa anatumika na Rais William Ruto kuzuia kasi ya harakati ya “One Term” (Kipindi Kimoja cha Uongozi).
Gachagua alisema kuwa wito wa Raila wa kuitishwa kwa kongamano la kitaifa la vizazi mbalimbali umejaa unafiki.
Raila Odinga Aikemea Amri ya Rais Ruto ya Kuwapiga Risasi Waandamanaji
“Nilisikia Raila Odinga akisema tuwe na mazungumzo, tuwe na kongamano la kitaifa, tujadiliane. Kilichotokea ni kwamba mzee ametumwa na Ruto ili kuleta mkanganyiko na kupunguza kasi ya harakati ya Wantam,” alisema Gachagua.
Alimkosoa Odinga kwa kushiriki mazungumzo na serikali ya sasa na zile zilizopita, akisema kuwa juhudi hizo hazijawahi kufanikisha makubaliano yoyote yaliyowekwa.
“Nilisikia akisema jana kuwa Riggy G si suluhu. Ndiyo, Riggy G si suluhu, sijawahi sema mimi ni suluhu, siwezi kuwa suluhu. Suluhu ni moja, ni kipindi kimoja tu. Huwezi kuizuia sasa ilipofikia, haiwezi kuzuiliwa,” Gachagua alisisitiza.
Aliendelea kudai kuwa kiongozi mmoja maarufu wa genge la uhalifu aliyekuwa akijulikana sana miaka ya 1990, na ambaye alikuwa akikabiliwa na kesi mahakamani, aliondolewa mashtaka kutokana na ushiriki wake katika machafuko ya maandamano ya hivi majuzi.
“Alikuwa na kesi ya uhalifu Makadara, ikafutwa ili ‘kumshukuru’ kwa kazi ‘nzuri’ aliyofanya,” alidai Gachagua.
Kiongozi huyo wa chama cha DCP aliendeleza ujumbe wake kuhusu harakati ya “Wantam” (Kipindi Kimoja), ambayo ni vuguvugu la kupinga serikali kwa lengo la kuzuia muungano wa Kenya Kwanza kupata kipindi cha pili madarakani.
“Wakenya wameamua, na si watu wa Mlima Kenya pekee, bali kote nchini asilimia 90 hawawezi kungoja. Ni kipindi kimoja tu,” alisema Gachagua.
Akiwa Seattle, Gachagua aliwahimiza Wakenya waishio ughaibuni kuendelea kutuma pesa nyumbani ili kusaidia kuimarisha uchumi.
“Chanzo kikuu cha mapato ya fedha za kigeni kwa nchi yetu ni pesa zinazotumwa na Wakenya wa diaspora. Ninyi ni washirika wetu muhimu sana katika maendeleo ya uchumi wetu,” alieleza Gachagua.