
Rais William Ruto amesema kuwa serikali yake tayari imechukua hatua mahsusi na makusudi katika kuunda nafasi za ajira.
Alisema hayo wakati wa kikao na maaskofu, wachungaji na wainjilisti kutoka Shirikisho la Makanisa ya Kieinjilisti na Kiasili ya Kikristo ya Kenya siku ya Jumatano,
“Vijana 400,000 wa Kenya wamepata ajira nje ya nchi katika kipindi cha miaka miwili iliyopita... Hapa nyumbani, vijana 320,000 wamehusika kikamilifu kupitia Mpango wa Makazi Nafuu," Ruto alisema.
“Wengine 180,000 wanajipatia kipato kupitia kazi za kidijitali katika Maabara za Jitume zilizoko katika vyuo vyetu vya kiufundi na katika Eneo Maalum la Kiuchumi la Tatu City. Uanzishaji wa vituo vya kidijitali katika wadi zetu 1,450 unaendelea.”
Ruto alisema kuwa serikali yake pia imeajiri walimu 76,000, na walimu wengine 24,000 wataajiriwa kufikia Januari 2026.
Hii ndiyo kampeni kubwa zaidi ya uajiri wa walimu katika historia ya nchi yetu.
Ruto alihimiza viongozi wa kanisa kushirikiana na serikali yake katika kutafuta suluhu kwa changamoto ya ukosefu wa ajira nchini.
Ruto alisema viongozi wanapaswa kujizuia dhidi ya kuwachochea vijana.
“Viongozi lazima wakatae kishawishi cha kuwachochea vijana. Badala yake, ni lazima tushirikiane kutafuta suluhisho la kudumu kwa changamoto ya ukosefu wa ajira,” alisema katika Ikulu ya Nairobi.
Matamshi yake yanakuja miezi michache baada ya baadhi ya viongozi wa kanisa kutoa kauli zilizoonekana kuunga mkono maandamano yaliyoongozwa na kizazi cha Gen Z nchini.
Viongozi hao pia walitoa wito wa kudumisha amani hata wakati vijana walipoeleza malalamiko yao.
Si mara ya kwanza kwa Ruto kuwaomba viongozi wa kanisa waunge mkono serikali yake.
Mbali na mikutano ya mara kwa mara na makundi mbalimbali ya viongozi wa kidini, Rais amesisitiza kuwa kanisa lina nafasi muhimu katika uongozi wa nchi.
“Kama serikali, tunatambua kazi ya kanisa na tunaheshimu mahali pa ibada. Nataka kuwahakikishia kuwa mahali pa ibada haitadunishwa,” alisema.
“Tunaenda kushirikiana na kanisa katika maeneo yote ya programu zetu za maendeleo. Pia tunawashukuru kwa mchango wenu katika sekta ya elimu na afya,” aliongeza.