logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Gachagua: Asilimia 80 ya Wakenya Wanaoishi Marekani Wanatoka Mlima Kenya

Aliitaja jamii hiyo kuwa na sifa ya kuwa na msukumo mkubwa katika biashara.

image
na Tony Mballa

Habari20 July 2025 - 13:29

Muhtasari


  • Alidai kuwa kushuka kwa uchumi kunachangiwa na hatua ya watu wengi kutoka Mlima Kenya kupunguza kwa makusudi ulipaji wa ushuru na uwekezaji, wakisubiri serikali itakayokuwa rafiki kwao.
  • Aliielezea jamii hiyo kama iliyoamua kushikilia rasilimali zake hadi pale hali ya kisiasa na kiuchumi itakapotengemaa.

Kiongozi wa Democracy for Citizens Party (DCP) Rigathi Gachagua amedai kuwa idadi kubwa ya Wakenya wanaoishi Marekani wanatoka katika eneo la Mlima Kenya, akisisitiza ushawishi mkubwa wa jamii hiyo ndani na nje ya nchi.

Akizungumza wakati wa mkutano na Wakenya waishio ughaibuni jijini Boston, Massachusetts mnamo Jumapili, Julai 20, 2025, Gachagua alieleza kuwa takriban asilimia 80 ya Wakenya walioko Marekani wanatoka Mlima Kenya.

“Nimefanya uchunguzi, na asilimia 80 ya Wakenya walioko Marekani ni watu kutoka milimani. Na hivyo ndivyo tulivyo. Sisi ni wachapa kazi na watu wa malengo,” alisema Gachagua.

Alisisitiza umuhimu wa jamii ya Mlima Kenya katika kuunda mwelekeo wa kijamii na kiuchumi wa Kenya, akiwataka wanaoishi ughaibuni kutambua ushawishi wao na kuendelea kuchangia maendeleo chanya.

Rigathi Gachagua

“Nataka mujitambue kuwa mna ushawishi mkubwa sana nyumbani,” aliongeza.

Katika hotuba hiyo hiyo, kiongozi huyo wa DCP alimshutumu waziwazi Rais William Ruto kwa kudhoofisha eneo la Mlima Kenya, akidai kuwa uhasama wa kisiasa dhidi ya eneo hilo umechangia kwa kiwango kikubwa kuyumba kwa uchumi wa taifa.

Gachagua alisema Mlima Kenya ndicho kiini cha uchumi wa Kenya, na alionya kuwa kudhoofisha biashara na wajasiriamali wa eneo hilo ni sawa na kuidhoofisha nchi nzima.

Alidai kuwa kushuka kwa uchumi kunachangiwa na hatua ya watu wengi kutoka Mlima Kenya kupunguza kwa makusudi ulipaji wa ushuru na uwekezaji, wakisubiri serikali itakayokuwa rafiki kwao.

Aliielezea jamii hiyo kama iliyoamua kushikilia rasilimali zake hadi pale hali ya kisiasa na kiuchumi itakapotengemaa.

“Ukivunja jamii hii, umeivunja Kenya. Sisi ndio tunaendesha uchumi wa nchi hii. Tangu William Ruto atangaze vita dhidi ya mlima, uchumi karibu umeanguka kwa sababu watu wameacha kulipa ushuru na kuwekeza wakisubiri serikali mpya.

"Kama mnavyoshikilia pesa zenu hapa, hata Kenya ndivyo watu wanavyofanya. Tunafanya biashara ndogo ndogo na kushikilia zingine tukisubiri uchumi kubadilika,” alisema Gachagua.

Pia alisifu bidii ya watu wa Mlima Kenya, akiwataja kuwa ni wajasiriamali wa hali ya juu na waliostahimili changamoto, iwe nyumbani au ughaibuni.

Aliitaja jamii hiyo kuwa na sifa ya kuwa na msukumo mkubwa katika biashara, na akasema si ajabu kwamba katika kila mji wa Kenya, mtu hupata mtu kutoka Mlima Kenya akiishi au akiendesha biashara.

“Hii ni jamii inayochochea ukuaji wa uchumi wa Kenya. Na ndiyo maana mnafanya vizuri hapa. Kwa sababu ndivyo tulivyozaliwa. Sisi ni watu wa kuchangamka, wajasiriamali na tunaopenda kusonga mbele, na ndiyo maana tupo kila mji wa Kenya. Na ndiyo maana mko hapa,” aliongeza.

Makala Zinazohusiana


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved