
LIMURU, KENYA, Julai 23, 2025 — Chama cha Democracy for Citizens Party (DCP) kinajipanga kwa mapokezi ya kihistoria kwa kiongozi wao Rigathi Gachagua, anapotarajiwa kurejea nchini baada ya ziara ya miezi miwili nchini Marekani.
Akihutubia mamia ya wafuasi katika mkutano wa hadhara uliofanyika Limuru, Seneta wa Kiambu Karungo wa Thang’wa alieleza kuwa DCP haitakubali Gachagua arejee kimya kimya.
“Tunaahidi tutarudi hapa tena, safari hii tukiwa na viongozi wote pamoja na Riggy G. Na akifika, lazima tuelekee moja kwa moja hadi uwanja wa ndege wa JKIA ili tumlete nyumbani kwa heshima anayostahili,” alitangaza Karungo huku akishangiliwa na umati.
Kauli hiyo imeonekana kama njia ya kuonyesha mshikamano na nguvu mpya ndani ya chama hicho, licha ya kuwepo kwa vuguvugu la kisiasa linaloendelea kufukuta nchini.
Gachagua aendelea kuwahutubia wafuasi kwa njia ya simu
Licha ya kutokuwepo nchini, Gachagua ameendeleza mawasiliano ya moja kwa moja na wafuasi wake kupitia simu, akizungumza nao moja kwa moja kutoka Marekani. Alifanya hivyo katika mkutano wa Subukia, Nakuru na kisha kurudia mtindo huo Limuru.
Ziara ya Gachagua ilianza rasmi Julai 10, 2025, na imeelezwa kuwa inalenga kuwafikia Wakenya walioko Marekani ambao wamefanikiwa lakini hawajarejea kusaidia jamii zao.
“Nimeenda Amerika kwa miezi miwili kuwatafuta ndugu zetu waliopotea kule miaka mingi iliyopita. Wamepata mafanikio makubwa lakini huku nyumbani tunahangaika. Nawaomba warudi, watusaidie, tupendane kama taifa,” alisema Gachagua katika mkutano wa awali Nyahururu mnamo Juni 29.
Serikali yakashifu matamshi yake
Ziara hiyo imezua taharuki baada ya Gachagua kudai kwamba watu wa karibu na Rais William Ruto walijaribu kumzuia kusafiri nje ya nchi na hata kutishia kumkamata uwanjani.
Tangu wakati huo, viongozi wa DCP wakiongozwa na naibu kiongozi Cleophas Malala wamezindua mikutano kadhaa ya kisiasa kote nchini, wakiendeleza ajenda ya chama hata akiwa nje ya nchi.
Hata hivyo, wanasiasa wa upande wa serikali wamemshutumu vikali Gachagua kwa kile walichokitaja kama "kueneza siasa za mgawanyiko na uchochezi ughaibuni."
Mpaka sasa, Gachagua ametembelea miji ya Boston na Seattle, na anatarajiwa kuelekea Texas katika siku chache zijazo, kabla ya kurejea nchini kwa kile kinachotajwa kuwa ni mapokezi ya aina yake.