NAIROBI, KENYA, Julai 30, 2025 — Kundi jipya lenye jina lenye mvuto wa kimataifa, Fighting Brutality and Impunity (FBI), limeanzishwa na watu watatu waliowahi kuhudumu katika vyombo vya ulinzi na usalama nchini na nje ya nchi. Lengo lao kuu: kupinga ukatili wa polisi na kutetea haki ya wananchi wa kawaida.
Kiongozi wa kundi hilo, Patrick Osoi, ambaye aliwahi kuwa mwanajeshi wa KDF Special Forces, afisa wa NIS na pia kuhudumia Jeshi la Marekani, alielezea dhamira yake kupitia mtandao wa X (zamani Twitter):
"Nikiwa nimehudumu kama mwanajeshi wa Kikosi Maalum cha KDF, afisa wa NIS na mkongwe wa Jeshi la Marekani, nimechukua jukumu la pamoja kuwakusanya maafisa wenzangu wanaoamini katika kupigania haki ya Wakenya."
Osoi alisema harakati yao inalenga kusaidia familia za waathiriwa wa operesheni kali za polisi, hususan waliopoteza wapendwa wao katika msako wa Juni 25, 2024, pamoja na maafisa waliotengwa na mfumo waliouhudumia kwa miaka.
"Wajibu wetu ni kuleta haki kwa watu wetu, na tutapambana kwa kila hali kuhakikisha tunafanikisha hilo."
Mwanaharakati mwingine ndani ya kundi hilo, Cop Shakur, ambaye ni afisa wa zamani wa polisi, alisema:
"Tutafanya uchunguzi wetu binafsi kuhusu mauaji ya kiholela na kuyarekodi."
Kauli hiyo inaonesha nia ya FBI kutafuta ushahidi huru wa dhuluma, pasipo kusubiri vyombo rasmi vya serikali.
Kwa upande wake, Hiram Kimathi, mtetezi wa haki na mageuzi ya kimfumo, alisema:
"Tumeungana kwa ajili ya jambo kubwa kuliko sisi wenyewe. Ni lazima tuiokoe nchi hii kutoka kwa dhuluma na ukosefu wa haki. Wanatam ni lazima."
Majibu Tofauti Mitandaoni:
Tangazo la FBI limesababisha mjadala mkubwa mitandaoni. Wapo waliolipokea kwa matumaini, lakini pia wengi walionyesha hofu na mashaka.
Mwingine, aliyejitambulisha kama Mr. Chairman, alidai kundi hilo linaweza kuwa tishio la kisiasa na akaonya kuhusu uwezekano wa serikali kulipiza kisasi.
Lakini wengine walionyesha matumaini. Gladwel Thiongo aliandika:
"Sisi ndio tunalalamikia ukatili wa polisi, lakini tunapowapata walio wema miongoni mwao, tunawadharau na kuwavunja moyo. Je, tunawatia moyo maafisa wema au tunawavunja kabisa?"
Mchango mwingine kutoka kwa mtumiaji aliyejitambulisha kama Kienje ulisomeka:
"Muda utaongea, ikiwa nyinyi ni kweli, basi Mungu mwenye nguvu awalinde na kuwaongoza."
Kipi Kinafuata?
Ingawa FBI bado haijatoa mkakati kamili wala ratiba ya shughuli zake, tayari uwepo wao umetikisa taswira ya harakati za kijamii nchini. Je, wataweza kushikilia msimamo wao mbele ya mashinikizo ya kisiasa na mitazamo ya umma?