NAIROBI, KENYA, Agosti 7, 2025 — Wingu jeusi limetanda kanyonyoo, kaunti ya Kitui, baada ya tukio la kikatili lililohusisha mauaji ya wanawake wawili, mmoja wao akiwa mke wa mtu, kwa risasi zinazodaiwa kufyatuliwa na afisa wa polisi aliyekuwa na uhusiano wa karibu na mmoja wao.
Joy Mutisya, mama wa watoto wawili na mke wa James Mutisya, aliondoka nyumbani wiki iliyopita akieleza kuwa alikuwa anaelekea Kitengela kutafuta kazi.
Hata hivyo, alielekea Kitui, ambapo alikutana na mwanamume anayesemekana kuwa mpenzi wake wa zamani — afisa wa polisi aliyekuwa akihudumu katika eneo la Kanyonyoo.
Siku chache baadaye, miili ya Joy na rafikiye Jane Ndanu ilipatikana katika makazi ya afisa huyo, kila mmoja akiwa amepigwa risasi.
Mshukiwa alikuwa ametoroka, huku silaha ya aina ya AK-47 ikikutwa imetupwa katika kichaka karibu na eneo la tukio.
Familia Yalia
Mume wa Joy, James Mutisya, bado yupo katika hali ya mshangao na majonzi. Kulingana na ndugu wa familia, hawakuwa na dalili zozote kwamba Joy alikuwa katika uhusiano wa nje ya ndoa au alikuwa hatarini.
"Joy alituaga vizuri, akisema anaenda kutafuta kazi. Hata hakusema Kitui. Sasa tunapokea mwili wake kwa risasi kichwani. Hili ni pigo ambalo familia haiwezi kufahamu," Jonathan Waema, baba mkwe wa marehemu, aliambia runinga ya Citizen.
Familia ya Jane Ndanu, aliyekuwa rafiki wa karibu wa Joy, pia wameachwa na maswali mengi. Kulingana na mashahidi, Jane alijaribu kumtetea Joy wakati wa ugomvi, ndipo naye akapigwa risasi.
“Askari alikuwa na hasira kali. Wote walikuwa ndani ya nyumba yake. Walianza kugombana, na tuliposikia kelele tukafika, tukakuta tayari wamepigwa risasi. Joy alikufa papo hapo, na Jane akafariki akiwa njiani hospitalini,” alisema Stanley Kiilu, jirani wa mshukiwa.
Polisi Wajibu
Kamanda wa Polisi Kaunti ya Kitui, Martha Nge’tich, amethibitisha kuwa tukio hilo lilihusisha afisa wao wa Kanyonyoo.
Ameeleza kuwa marehemu Joy alikuwa na uhusiano wa karibu na mshukiwa, na kwamba walikuwa wamegombana kabla ya tukio hilo kutokea.
"Ni kweli kulikuwa na mzozo wa kimapenzi. Marehemu alikuwa ndani ya nyumba ya afisa huyo kwa muda wa siku mbili. Uhasama ulianza usiku wa tukio hilo, na baadaye tukapokea taarifa kuwa kuna watu waliouawa," alisema Nge’tich.
Polisi kwa sasa wanamsaka afisa huyo, ambaye alitoroka na bado hajapatikana. Wametangaza kuwa yeyote mwenye taarifa za aliko mshukiwa anaombwa kutoa taarifa kwa kituo cha polisi kilicho karibu.
Wito Wa Haki
Huku familia zikijiandaa kwa mazishi ya wapendwa wao, sauti za kilio cha haki zinazidi kupaa. Wazazi wa Joy na Jane wameitaka serikali kuhakikisha mshukiwa anatiwa mbaroni haraka na akabiliwe na mkono wa sheria.
“Tunataka haki kwa watoto wetu. Polisi hawa waliletwa kutulinda, lakini sasa wanatunyanyasa na kutuua. Ikiwa huyu afisa hatakamatwa, basi sisi kama familia hatutakubali. Serikali ichukue hatua,” alisema Peter Mwania, jamaa wa familia ya marehemu.
Miili Yachukuliwa, Uchunguzi Wa Maiti Kusubiri
Miili ya Joy na Jane imehifadhiwa katika mochari ya Hospitali ya Kitui ikisubiri kufanyiwa upasuaji wa maiti.
Uchunguzi huu unatarajiwa kutoa picha kamili ya madhila yaliyowakumba kabla ya mauti yao.
Tayari maandalizi ya mazishi yameanza katika kijiji cha Kwa Mwania, huku waombolezaji wakiendelea kumiminika kutoa pole kwa familia.