
LONDON, UINGEREZA, Ijumaa, Oktoba 3, 2025 – Klabu ya Arsenal inatarajiwa kushuka dimbani Emirates Stadium Jumamosi saa kumi alasiri kwa mchezo wa Ligi Kuu England dhidi ya West Ham United.
Makocha Mikel Arteta na Nuno Espirito Santo wanakutana kwa mara ya kwanza katika dabi hii ya London yenye ushindani mkubwa.
Arsenal imekuwa na changamoto dhidi ya West Ham katika michezo ya nyumbani. Katika mechi nne za mwisho Emirates, Gunners wamepoteza mara mbili kwa Hammers.
Ikiwa West Ham watashinda tena, watakuwa timu ya pili pekee katika historia ya ligi kushinda mara tatu mfululizo ugenini dhidi ya Arsenal.
Kauli za makocha

Kocha wa Arsenal amesema anataka timu yake kuvunja nuksi ya kupoteza mara mbili mfululizo dhidi ya West Ham nyumbani.
“Tunataka kuendelea kucheza kwa kasi na kushinda mechi muhimu. Tunajua West Ham ni wapinzani wagumu na tunahitaji kujibu changamoto hii,” amesema Arteta.
Ameongeza kuwa mashabiki wanatarajia matokeo chanya: “Tunajua wanataka ushindi, na jukumu letu ni kuhakikisha tunawapa sababu ya kufurahia.”
Nuno Espirito Santo

Kocha mpya wa West Ham amesema anataka kikosi chake kuonyesha mshikamano. “Kila mtu ndani ya klabu amejitolea.
Tunapaswa kucheza kwa ujasiri na nidhamu. Tunahitaji kuwa imara na kushindana katika kila dakika,” amesema Nuno.
Ameongeza kuwa mashabiki ni nguvu ya timu: “Tunapotembea na mashabiki nyuma yetu, wachezaji wanajisikia huru. Tunataka kuwarudishia furaha kupitia matokeo.”
Habari za majeruhi
Arsenal huenda wakakosa beki Gabriel ambaye alitolewa uwanjani dhidi ya Olympiacos. Hincapie bado anauguza jeraha la groin, huku Havertz, Jesus na Madueke wakiwa nje. Kwa West Ham, Tomas Soucek atakosa mechi kwa sababu ya kadi nyekundu, na chipukizi George Earthy ameumia paja.
PICHA YA JALADA: Wachezaji wa Arsenal washerehekea bao lao/ARSENAL FACEBOOK