
Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna asema chama hicho kitasimamisha mgombea wake wa urais mwaka 2027, kikiahidi kuendeleza urithi wa Raila Odinga na kulinda uthabiti wake kisiasa.
Chama cha Orange Democratic Movement (ODM) kimethibitisha rasmi kuwa kitasimamisha mgombea wake wa urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2027, hatua inayosisitiza msimamo wake wa kujitegemea na kulinda urithi wa kisiasa wa marehemu Raila Amolo Odinga.
Katibu Mkuu wa ODM na Seneta wa Nairobi, Edwin Sifuna, alitoa tamko hilo Ijumaa akithibitisha kuwa maadhimisho ya miaka 20 ya ODM yatafanyika kama ilivyopangwa mjini Mombasa kuanzia Novemba 14, na kwamba tukio hilo litakuwa pia kumbukumbu maalum ya kumuenzi kiongozi huyo wa chama.
“Tutajitosa Peke Yetu,” Asema Sifuna
Sifuna alifafanua kuwa ODM haitajiunga na muungano wa vyama vingine kwa ajili ya urais, akisema chama hicho kina nguvu ya kutosha kushinda uchaguzi kwa tiketi yake.
“Tutasimama kivyetuvyetu kama ODM. Msidanganywe kwamba tutakuwa na mgombea wa pamoja, kwa sababu hakuna chama kinachoitwa ‘broad-based’,” alisema Sifuna kwa msisitizo.
Aliongeza kuwa ODM imejijenga kwa misingi imara ya uaminifu na ushawishi wa kitaifa.
“Nikuambie, kama ni Sifuna au mtu mwingine yeyote atasimama kwa tiketi ya ODM, naamini atashinda urais mwaka 2027. Mimi ni mwaminifu kwa ODM. Kuifanya chama iwe imara kama ODM si jambo rahisi, na ndiyo maana nitaendelea kuwa mwanachama wake,” aliongeza.
Sifuna Atoa Onyo kwa Wanaodai Kushauriwa na Raila
Sifuna pia alikemea wanasiasa wanaodai kuwa marehemu Raila Odinga aliwapa maelekezo binafsi kuhusu mustakabali wa chama kabla ya kifo chake.
“Kila mtu anadai alifahamishwa na Baba. Ukweli ni kwamba hadithi ya kuaminika ni ile aliyoitoa mbele ya wabunge wengi, akisema wazi kuwa ODM itakuwa na mgombea wake wa urais mwaka 2027,” alisema Sifuna.
Kauli hiyo ilipokelewa kwa shangwe kutoka kwa wajumbe waliokuwa wamekusanyika Mombasa, wakisema imeweka wazi mwelekeo wa chama baada ya kipindi cha sintofahamu.
Oburu Odinga: ODM Haitapoteza Utambulisho Wake
Kaimu kiongozi wa chama cha ODM na Seneta wa Siaya, Oburu Odinga, alisisitiza kuwa ODM inajiandaa kuunda serikali ijayo na haitapoteza utambulisho wake licha ya ushirikiano na serikali iliyo madarakani.
“ODM haitabadilika rangi kwa sababu ya ushirika. Hakuna mtu atakayekuheshimu bila kuwa na idadi kubwa ya wafuasi. Ndiyo maana tunapaswa kubaki ndani ya chama. Wakiwapa pesa, chukueni, lakini mioyo yenu ibaki ODM,” alisema Oburu.
Alimshukuru Gavana wa Mombasa Abdulswamad Sherrif Nassir kwa kumpendekeza kuwa kaimu kiongozi wa chama, akieleza safari yake ndefu ya kisiasa.
“Ninahudumu kwa muhula wangu wa saba bungeni. Nilianza mwaka 1974 kama diwani Kisumu, nikawa Mbunge wa Bondo, Mbunge wa EALA, nikateuliwa mara moja, na sasa ni Seneta wa Siaya. Hii inaonyesha ninastahili kuongoza ODM,” alisema.
“Nilimpenda Kaka Yangu Raila” – Oburu Akumbuka
Oburu alionekana kuguswa sana alipozungumzia kifo cha kaka yake, akisema Raila hakuwa tu ndugu yake bali pia rafiki na mshauri mkubwa.
“Kifo cha kaka yangu kiliniumiza sana kwa sababu tulikua pamoja, tulishauriana mambo mengi. Raila hakuwa tu ndugu yangu bali alikuwa mshauri wangu,” alisema kwa huzuni.
Wajumbe walisimama kwa dakika moja kuonyesha heshima zao kwa Raila Odinga, wakiimba wimbo wa “ODM Haiwezi Kufa” kama ishara ya uhai wa urithi wake.
Nassir: ODM Inataka Kiti cha Urais
Naibu Kiongozi wa ODM na Gavana wa Mombasa, Abdulswamad Sherrif Nassir, aliwataka wanachama waendelee kuwa imara na waaminifu kwa chama, akisema wakati wa ODM kubaki upande wa upinzani umekwisha.
“ODM haitakuwa tena chama cha upinzani. Tunaandaa miundombinu yetu, tunajipanga kushinda urais mwaka 2027 au kuwa sehemu ya serikali ijayo. Hatuprinti fulana na kufanya mikutano yote hii bure. Tunataka kiti cha juu,” alisema Nassir.
Aliongeza kuwa ODM ndiyo chama chenye mtandao mpana zaidi nchini, hasa miongoni mwa vijana, na ndicho kinachoweza kuleta mageuzi ya kweli ya kisiasa.
Mombasa Kuwaka Moto kwa Sherehe za Miaka 20 ya ODM
Maandalizi ya maadhimisho ya miaka 20 ya ODM mjini Mombasa yamekamilika, yakitarajiwa kuvutia maelfu ya wajumbe kutoka kaunti zote. Tukio hilo litajumuisha kumbukumbu ya Raila Odinga, mijadala ya kisiasa, na mikakati ya kampeni za mwaka 2027.
Sifuna alisema maadhimisho hayo yatakuwa “sherehe ya uthabiti, uongozi na moyo wa chama ambacho kimehimili dhoruba kwa miaka ishirini bila kuyumba.”
Safari Mpya ya ODM
Kadiri chama cha ODM kinapoelekea kuadhimisha miaka 20 tangu kuanzishwa kwake, kinaingia katika enzi mpya yenye changamoto na matumaini.
Urithi wa Raila Odinga bado unaleta mwanga, huku viongozi wapya kama Sifuna, Oburu na Nassir wakichukua jukumu la kuendeleza mwenge huo wa kisiasa.
Iwapo ODM itafika Ikulu mwaka 2027 bado ni swali, lakini ujumbe kutoka Mombasa ni wazi: chama cha machungwa hakijalala – kinaamka tena kupigania ushindi.




© Radio Jambo 2024. All rights reserved