
MURANG'A, KENYA, Jumanne, Januari 13, 2026 – Mbunge wa Kiharu, Ndindi Nyoro, ametangaza punguzo kubwa la karo kwa shule za upili za kutwa katika eneo lake, hatua inayolenga kupunguza mzigo wa gharama za elimu kwa wazazi na kuongeza fursa za masomo kwa wanafunzi.
Kupitia mpango wa Kiharu Masomo Bora 2026, karo ya shule za upili za kutwa imepunguzwa kutoka Sh1,000 hadi Sh500 kwa muhula kwa wanafunzi wote kuanzia Gredi ya 10 hadi Kidato cha Nne.
Hatua hiyo inatarajiwa kunufaisha zaidi ya wanafunzi 12,000 wanaosomea katika shule 65 za upili za kutwa ndani ya eneo bunge hilo.
Muundo mpya wa karo utaanza kutekelezwa kuanzia Muhula wa Kwanza wa 2026 na utawahusu wanafunzi wote wa shule za upili za kutwa za umma katika Kiharu.
Mpango wa chakula shuleni waanzishwa
Mbali na punguzo la karo, mpango huo umeanzisha mpango kabambe wa lishe shuleni, ambapo wanafunzi wote watapatiwa chakula cha mchana siku zote za masomo, ikiwemo Jumamosi.
Ratiba ya mlo itajumuisha githeri kwa siku tatu kwa wiki, wali kwa siku tatu, pamoja na uji wakati wa mapumziko ya chai, huku chapati ikitolewa Ijumaa ya mwisho wa kila mwezi. Hatua hiyo inalenga kuboresha mahudhurio, umakini darasani na ufaulu wa wanafunzi.
Mamilioni ya shilingi kwa vifaa na miundombinu
Katika kuimarisha ubora wa masomo, NG-CDF ya Kiharu imetenga Sh10 milioni zaidi kwa ajili ya vifaa vya marudio katika mwaka wa sasa wa kifedha, juu ya Sh20 milioni zilizowekezwa katika miaka ya awali.
Zaidi ya Sh50 milioni pia zimetumika kuboresha miundombinu ya shule, kwa msisitizo mkubwa ukiwekwa katika ujenzi na uboreshaji wa maabara.
Sare za bure na fedha za shughuli za ziada
Wanafunzi wanaojiunga na Gredi ya 10 katika shule 20 zilizotambuliwa kuwa na idadi ndogo ya wanafunzi au zilizoanzishwa hivi karibuni watapatiwa sare za shule bila malipo.
Aidha, kila moja ya shule 65 za upili za kutwa itapokea Sh50,000 kusaidia shughuli za muziki, michezo na shughuli nyingine za ziada.
Motisha kwa walimu na wakuu wa shule
Mpango huo pia umeweka motisha kwa walimu na wasimamizi wa shule, ambapo mwalimu bora katika kila kata ndogo atalipiwa safari ya Mombasa.
Kwa upande mwingine, wakuu wa shule watakaofanya vyema zaidi watapewa zawadi za safari za kimataifa kwenda Dubai au Malaysia.
Ada za ziada zapigwa marufuku
Shule zitakazoruhusiwa kuendesha programu za masomo ya ziada (remedial) zitaruhusiwa kutoza kiwango cha juu cha Sh1,000 kwa muhula pekee.
Ada nyingine zozote za usajili au malipo ya ziada zimepigwa marufuku katika shule zote zitakazonufaika na mpango huo.
Bima na matengenezo ya mabasi kugharamiwa
Kadhalika, bima na gharama za matengenezo ya mabasi ya shule yanayomilikiwa na shule za upili za kutwa zitagharamiwa chini ya mpango huo, hatua itakayopunguza mzigo wa kifedha kwa shule na wazazi.
Mpango wa Kiharu Masomo Bora 2026 unawahusu wanafunzi wote, wakiwemo wale wanaotoka nje ya Kiharu, mradi tu wamesajiliwa katika shule za upili za kutwa ndani ya eneo bunge hilo.


