

Oketch Salah, mwana wa kulelewa wa Waziri Mkuu wa zamani marehemu Raila Odinga, amevunja ukimya wake kufuatia mijadala na madai yanayoendelea kwenye mitandao ya kijamii kuhusu siku za mwisho za maisha ya Baba Raila, akisisitiza kwamba alikuwa naye tangu alipoanza kuugua hadi pumzi yake ya mwisho.
Katika taarifa ndefu iliyojaa hisia nzito, Salah alisema ameamua kuzungumza kwa mara ya kwanza kwa sababu jina lake limekuwa likitajwa mara kwa mara katika mijadala aliyodai imejaa upotoshaji, chuki na masimulizi ya kubuni.
“Mimi ndiye ninayelaumiwa, kwa hivyo nitajibu moja kwa moja na kwa utulivu,” alisema Salah.
Alisema kauli yake haikusudiwi kutafuta huruma, umaarufu wala faida ya kisiasa, bali kulinda ukweli kuhusu kipindi cha mwisho cha maisha ya kiongozi huyo mashuhuri wa kitaifa.
“Nilikuwa Naye Kuanzia Mwanzo wa Ugonjwa”
Salah alithibitisha kuwa alikuwa karibu na Raila Odinga tangu alipougua mara ya kwanza, hadi alipofariki dunia, akielezea kipindi hicho kama cha mateso makubwa ya kihisia.
“Nilikuwa na Baba Raila Odinga tangu alipoanza kuugua hadi alipovuta pumzi yake ya mwisho. Huo ni ukweli,” alisema.
Alisimulia kuwa kulikuwa na nyakati ngumu sana ambapo hali ya Baba Raila ilizorota ghafla, kiasi cha kumfanya ahofie maisha yake.
“Kulikuwa na wakati nilihisi kabisa kuwa namkosa Baba. Kulikuwa na wakati mimi na askari mmoja wa usalama tulikuwa peke yetu, nikimshika, nikijaribu kumtuliza na kumsaidia kuvumilia maumivu,” alisema.
Alifafanua kuwa askari huyo wa usalama hakuwa Maurice Ogetta, akikanusha madai yaliyosambaa mitandaoni.
Mazungumzo ya Faragha na Heshima ya Kimya
Kwa mujibu wa Salah, kipindi hicho kilimpa nafasi ya kuwa na mazungumzo mengi na Raila Odinga, yakiwemo ya binafsi, kisiasa na ya kimkakati.
“Tulikuwa na mazungumzo mengi; ya binafsi, ya kisiasa na ya kimkakati, mengi ambayo Baba alichagua kuyaendesha nami kwa faragha,” alisema.
Hata hivyo, Salah alisema hatatoa maelezo ya mazungumzo hayo kwa heshima ya marehemu na familia yake.
“Kwa heshima yake na familia yake, sitafichua mazungumzo hayo. Kimya kisiwe tafsiri ya woga au uongo,” alisema.
Kanusho la Kumdharau Mama Ida na Familia
Salah alikanusha vikali madai kuwa alijaribu kujipa nafasi ya familia ya Raila Odinga au kuwadharau Mama Ida Odinga na watoto wake.
“Sijawahi kudai kuchukua nafasi ya familia ya Baba wala sijawahi kumdharau Mama Ida au watoto wake,” alisema.
Alisema madai hayo ni ya uongo, ya chuki na yenye nia mbaya.
“Madai kuwa niliwatukana, niliwatenga au kuwasemea vibaya ni ya uongo mtupu. Nayakataa kabisa,” aliongeza.
Tayari Kujitokeza Hadharani
Akijibu hoja kuwa amekuwa akijificha, Salah alisema hana hofu ya kuhojiwa au kuchunguzwa.
“Sina hofu ya uchunguzi. Niko tayari kuhojiwa hadharani, wakati wowote, katika jukwaa lolote lenye uaminifu,” alisema.
Alisisitiza kuwa ukweli hauogopi kuulizwa maswali.
“Ukweli hauogopi uchunguzi,” aliongeza.
Kwa msimamo mkali, Salah alisema hatakubali kubebeshwa lawama ili wengine wapambane vita zao za ndani au kuandika upya historia ya maisha ya Raila Odinga.
“Sitakubali kufanywa mhusika wa kulaumiwa ili wengine wapigane vita zao za ndani au waandike upya historia ya maisha halisi,” alisema.
Alisisitiza kuwa hakujiingiza kwa nguvu katika maisha ya Baba Raila.
“Nilikuwepo kwa sababu Baba aliniruhusu kuwepo, kwa hiari yake na kwa ufahamu kamili,” alisema.
Wito wa Heshima kwa Maombolezo
Katika kauli yake ya mwisho, Salah aliwataka Wakenya kupunguza mashambulizi na makelele ya mitandaoni, akisema huzuni haifai kugeuzwa burudani au silaha ya kisiasa.
“So bwana wacheni, hamuelewi. Wallahi,” alisema.
Aliongeza kuwa si kila jambo linafaa kugeuzwa mjadala wa mitandaoni.
“Kuna mambo si ya makelele, si ya timelines wala si ya propaganda. Maumivu yanahitaji heshima, siyo tamasha,” alisema.
Kauli ya Salah imezidisha mjadala mpana kuhusu urithi wa Raila Odinga, mmoja wa viongozi waliotikisa siasa za Kenya kwa miongo mingi.
Wachambuzi wa siasa wanasema kifo cha Raila kimeacha pengo kubwa la kisiasa na kihisia, huku simulizi tofauti zikiibuka kuhusu siku zake za mwisho.
Huku mjadala ukiendelea, Salah amesema hatavurugwa na mashambulizi ya mtandaoni wala maigizo ya kisiasa.
“Ninajua niliposimama. Najua nilichofanya. Najua Baba alichoniamini nacho. Ukweli huo hauwezi kubadilishwa na makundi ya mtandaoni,” alisema.



