
Kiongozi wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM), Oburu Oginga, amepuuzilia mbali madai ya kuwepo kwa ushindani wa kisiasa kati ya chama chake na Naibu Rais, akisisitiza kuwa ushirikiano wa ODM na serikali ya Rais William Ruto unaongozwa na maslahi ya kitaifa, si tamaa ya madaraka.
Akizungumza Jumatatu wakati wa uzinduzi wa mpango wa Nota mjini Kisumu, Oburu alisema ODM haina nia ya kutikisa serikali wala kunyakua viti vya uongozi, bali inalenga kuhakikisha Wakenya wanapata maendeleo na huduma wanazostahili.

“Kwa Naibu Rais, hatutaki kiti chako. Wewe ni rafiki yetu,” alisema Oburu. “Tunapoketi mezani, tunajadili kile kinachowafaa watu wetu na Wakenya wote.”
Kauli hiyo imejiri huku mijadala ikiendelea kuhusu nafasi ya ODM ndani ya serikali jumuishi na mwelekeo wa chama hicho katika siasa za kitaifa.
Ushirikiano wa ODM na Kenya Kwanza
Oburu alitetea uamuzi wa ODM kushirikiana na utawala wa Kenya Kwanza, akisema ulikuwa uamuzi wa kimkakati baada ya miaka mingi ya siasa za upinzani na misukosuko ya kitaifa.
Alieleza kuwa mazingira ya kisiasa yalibadilika pakubwa baada ya chama kupoteza baadhi ya nguzo zake za kihistoria, hali iliyolazimu ODM kutathmini upya nafasi yake katika ujenzi wa taifa.
“ODM imeshirikiana na UDA katika serikali jumuishi. Tangu tulipopoteza kaka yangu na akaondoka akatuacha katika hali hii, tuliamua tushirikiane,” alisema.
Kwa mujibu wa Oburu, ushirikiano huo hauashirii kusaliti misingi ya chama, bali ni njia ya kuhakikisha sauti ya wananchi inaendelea kusikika serikalini.
Onyo Kuhusu Maandamano
Akijibu wito wa baadhi ya viongozi wa upinzani wa kurejea mitaani, Oburu alitoa onyo kali dhidi ya kuchochea maandamano yasiyo na mwelekeo.
Alisema wafuasi wa ODM wanafahamu gharama ya maandamano, ikiwemo vifo, uharibifu wa mali na kuyumba kwa uchumi.
“Sisi tulijulikana kwa maandamano. Wengine sasa wanaanza kusema maandamano — waache waje, tutawaonyesha maandamano. Hawajui maandamano,” alisema.
Aliongeza kuwa maandamano bila mkakati wa kisiasa na mazungumzo ya kweli yanaweza kuirejesha nchi nyuma.
ODM ni Chama cha Kitaifa
Oburu pia alikanusha madai kuwa ODM ni chama cha kikabila au cha eneo moja.
Alisisitiza kuwa ODM ni chama cha kitaifa chenye wanachama kutoka pembe zote za nchi.
“Chama chetu si cha Wajaluo. Ni chama cha nchi nzima,” alisema.
Aliongeza kuwa ajenda kuu ya ODM ndani ya serikali jumuishi ni usawa wa maendeleo na mgawanyo wa haki wa rasilimali za taifa.
“Tutaakikisha kila mtu anapata sehemu yake ya keki ya taifa,” alisisitiza.
Duru kwa Wapinzani Wapya wa Kisiasa
Katika hotuba yake, Oburu alielekeza dongo kwa wanasiasa wanaojipanga kuwania uongozi wa taifa, akisema hawajaonekana kuungana na wananchi wala kufanya kampeni za kitaifa.
“Wanaotaka kuchukua serikali — siwaoni wakifanya kampeni. Wanazunguka eneo moja tu,” alisema.
Kwa upande mwingine, alimpongeza Rais William Ruto kwa bidii yake ya kisiasa, akisema hajawahi kushuhudia rais mwenye kasi na juhudi kama hizo.
“Sijawahi kuona rais akifanya siasa kwa nguvu kama hii,” alisema.
Wito wa Umoja na Utulivu
Oburu aliwahimiza Wakenya kuunga mkono mshikamano wa kisiasa ili kufungua fursa za maendeleo na ustawi wa pamoja.
Alisema siasa za migawanyiko zinavuruga juhudi za kushughulikia changamoto kuu kama gharama ya maisha, ajira na huduma za kijamii.
“Tukumbatie nchi yetu ili watu wetu wanufaike,” alisema.
Alimalizia kwa msemo uliovutia wengi: “Tufike Kanaani kupitia Singapore,” akimaanisha maendeleo yafikiwe kwa nidhamu, subira na busara.
Upinzani Walalamikia Ghasia
Kauli za Oburu zimekuja wakati ambapo baadhi ya viongozi wa upinzani wameeleza wasiwasi kuhusu visa vya vurugu na usumbufu katika mikutano yao ya kisiasa.
Wiki jana, viongozi hao walisema wanawasilisha malalamishi rasmi kwa vyombo vya usalama ili kuhakikisha shughuli zao zijazo zinafanyika kwa usalama.
Walisisitiza kuwa uhuru wa kisiasa na mikutano ya amani ni haki ya kikatiba.
Gachagua Atishia Maandamano ya Kitaifa
Akizungumza na wanahabari katika eneo la Biashara, Nairobi, Ijumaa, aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua alisema upinzani umewasilisha ushahidi wa visa vya vurugu kwa Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja.
Alionya kuwa hatua zikikosekana, upinzani utawahamasisha Wakenya kuandamana.
“Tumepeleka maelezo kwa Inspekta Jenerali achukue hatua dhidi ya waliohusika,” alisema. “Ikiwa hakuna hatua itakayochukuliwa, tutawahimiza Wakenya watoke nje.”
Mizani Nyeti ya Kisiasa
Kauli za Oburu Oginga zinaangazia mizani nyeti ambayo ODM inalazimika kucheza huku ikishirikiana na serikali na wakati huo huo ikilinda misingi yake ya kisiasa.
Kadri joto la kisiasa linavyozidi kupanda, msimamo wa ODM unaashiria mwelekeo wa mazungumzo, utulivu na maendeleo badala ya shinikizo la mitaani.
Iwapo msimamo huo utaendelea kudumu au la, litabaki kuwa swali kuu katika mwelekeo wa siasa za Kenya miezi ijayo.



