logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Karen Nyamu afunguka alivyokutana na mpenzi wake Samidoh, kwa nini huwa anampigania

Karen Nyamu amefichua kwamba amekuwa kwenye mahusiano na mwimbaji Samidoh kwa takriban miaka mitano.

image
na Radio Jambo

Yanayojiri23 July 2023 - 06:03

Muhtasari


•Karen Nyamu amefichua kwamba amekuwa kwenye mahusiano na mwimbaji Samidoh kwa takriban miaka mitano.

•Nyamu amekana madai ya kuvunja ndoa ya Samidoh na ya 'kumuiba' mwimbaji huyo wa Mugithi kutoka kwa mkewe wa miaka mingi, Edday Nderitu.

Seneta wa kuteuliwa Karen Nyamu amefichua kwamba amekuwa kwenye mahusiano na mwimbaji Samuel Muchoki almaarufu Samidoh kwa takriban miaka mitano.

Katika mahojiano na Ala C kwenye kipindi cha Reke Ciume na Ene, mama huyo wa watoto watatu alifichua kwamba alikutana na baba huyo wa watoto wake wawili wadogo katika shughuli za kisiasa.

Hata hivyo, alikanusha madai kwamba waliunganishwa pamoja na mfanyibiashara Mike Sonko kama alivyodai gavana huyo wa zamani wa Nairobi katika siku za nyuma. 

"Sonko alidhani hivyo (alikuwa ametuunganisha), lakini hata wakati ule tukiwa Dubai tulikuwa tunajuana. Sonko alikuwa bosi wangu, nililazimika kumficha white. Nilikuwa nimeficha white kwa hiyo alidhani yeye ndiye aliyefanya hivyo, kumbe tulikuwa tumezungumza (na Samidoh)," Nyamu alisema.

Seneta huyo wa UDA pia alikanusha madai ya kuvunja ndoa ya Samidoh na ya 'kumuiba' mwimbaji huyo wa Mugithi kutoka kwa mkewe wa miaka mingi, Edday Nderitu.

“Sijawahi kumuibia mtu mume, tena huyo mwanaume, nina watoto naye na anapenda watoto. Ukitaka kugombana na kutofautiana naye, jaribu kumtenga na watoto wake, wote,” alisema.

Nyamu alidokeza kuwa mzazi mwenzake ameweza kutunza nyumba zake zote mbili, yake na ya Edday Nderitu kwa miaka mingi.

Aidha, alidokeza kwamba licha ya drama zote katika maisha yake ya mahusiano, yeye ni mwanamke mwaminifu sana na huwa anampigania tu Samidoh kwa sababu ni baba wa watoto wake.

Mwanasiasa huyo aliyezingira na drama alibainisha kwamba yeye huwa hasababishi fujo kwa sababu ya mapenzi bali kwa sababu anataka watoto wake wajisikie kuwa wanatambulika.

"Watoto wangu wanakua katika mazingira hayo, hakuna wakati nitaruhusu watoto wangu wajisikie kama watoto wadogo kuliko wengine, kwamba watoto wangu hawawezi kupostiwa na baba yao lakini wengine wanaweza kupostiwa ilhali wanamjua baba yao na wana uhusiano. Nataka kurekebisha mazingira ya watoto wangu iwezekanavyo ili wawe na wazazi wanaowapenda hadi wakati ambao haitawezekana tena, ikiwa wakati huo utafika, nitakuwa nimejaribu kila wakati hivyo sitajuta," alisema.

Nyamu alisisitiza kwamba kamwe huwa hahusiki katika vita na mkewe Samidoh, Bi Edday Nderitu au kujibizana naye hata anapochokozwa.

"Chochote unachoweza kusikia nikizungumza juu yake ni kitu kizuri," alisema.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved