logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Rais wa Afrika Kusini atia saini sheria yenye utata ya kunyakua ardhi

Serikali imesema sheria hiyo "inafafanua jinsi kupokonywa ardhi kunaweza kufanyika na kwa misingi gani."

image
na BBC NEWS

Kimataifa26 January 2025 - 08:12

Muhtasari


  • Rais Ramaphosa ametia saini sheria inayoruhusu serikali kunyakua ardhi kutoka kwa wazungu bila kutoa fidia,
  • Sheria hii imetangazwa baada ya mchakato wa mashauriano wa miaka mitano pamoja na mapendekezo ya kamati maalum


Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini, ametia saini sheria inayoruhusu serikali kunyakua ardhi kutoka kwa wazungu bila kutoa fidia, hatua ambayo imezua mzozo mkali ndani ya serikali yake.

Zaidi ya miaka 30 baada ya kumalizika kwa mfumo wa ubaguzi wa rangi, waafrika kusini weusi wanamiliki sehemu ndogo tu ya ardhi ya kilimo nchini mwao, huku sehemu kubwa ikibaki mikononi mwa walowezi wachache wazungu.

Serikali imesema sheria hiyo "inafafanua jinsi kupokonywa ardhi kunaweza kufanyika na kwa misingi gani."

Sheria mpya inachukua nafasi ya sheria ya awali ya Upokonyaji wa mashamba ya mwaka 1975, iliyokuwa ikiilazimisha serikali kulipa fidia wamiliki wa ardhi waliokuwa tayari kuuza mali zao kwa mfumo wa "muuzaji na mnunuzi aliyeridhia." Mfumo huo umeleta hasira na kufadhaika kutokana na kasi ndogo ya mabadiliko katika umiliki wa ardhi.

Chama cha ANC cha Ramaphosa kimepongeza sheria hiyo kama hatua muhimu katika mageuzi ya nchi, lakini baadhi ya wanachama wa serikali ya muungano wametishia kuipinga mahakamani. Sheria mpya inaruhusu serikali kuchukua ardhi bila fidiaikiwa itakuwa "ya haki na sawa" na kwa maslahi ya umma.

Msemaji wa Rais, Vincent Magwenya, alisema kuwa chini ya sheria hiyo, "serikali haiwezi kunyakua mali ya watu kiholela au kwa sababu nyingine yoyote isipokuwa kwa maslahi ya umma."

"Kunyang'anywa mali hakuwezi kufanyika isipokuwa mamlaka husika itajaribu bila mafanikio kufikia makubaliano na mmiliki," aliongeza.

Sheria hii imetangazwa baada ya mchakato wa mashauriano wa miaka mitano pamoja na mapendekezo ya kamati maalum ya rais iliyoundwa kuchunguza suala hili.



RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved