TAKRIBANI miezi 11 tu baada ya kuondoka ofisini, rais wa zamani wa Nigeria, Muhammadu Buhari amezua mjadala baada ya kukiri kwamba yeye si tajiri.
Rais huyo mstaafu aliwashangaza wengi
alipoungama kwamba baada ya kumaliza miaka 8 ya urais, sasa anaishi maisha ya
kutegemea kodi za nyumba kutoka kwa wapangaji wake.
Muhammadu Buhari alisema kuwa
familia yake sasa inategemea mapato kutokana na kupangisha moja ya nyumba zake
mbili katika Jimbo la Kaduna, akisisitiza kuwa "sikujitajirisha kwa rushwa
kama rais."
Kwa mujibu wa Sahara Reporters, Buhari
alitoa madai haya alipokuwa akihutubia mkutano wa wanachama wa All Progressive
Congress (APC) katika Jimbo la Katsina siku ya Jumapili, kabla ya uchaguzi wa
baraza la mtaa wa jimbo hilo uliopangwa kufanyika Februari 15.
Alisisitiza kuwa aliondoka
madarakani bila utajiri wowote alioupata kinyume cha sheria, akibainisha kuwa
Nigeria ni nchi ngumu kutawala kutokana na ugumu wake.
Akizungumza kwa lugha ya Kihausa,
rais huyo wa zamani alisema kuwa Wanigeria wengi hawakufahamu changamoto za
kiutawala zinazohusika katika kutawala nchi, lakini wanalaumu tu viongozi.
"Nigeria ni nchi ngumu
kutawala, lakini Wanigeria wengi hawajui. Mpaka ujipate katika nafasi ya
utawala wa nchi, ikiwa sivyo, huwezi kuelewa magumu.”
“Naonekana bora na mwenye afya
tele sasa kuliko nilipokuwa rais wa nchi. Yeyote anayeniona sasa anakubali kuwa
ninaonekana bora kuliko hapo awali," Buhari alisema.
Aliongeza, “Baada ya miaka minane nikiwa
rais wa serikali, nina nyumba tatu tu; moja huko Daura na mbili Kaduna. Nimetoa
moja kwa ajili ya kukodisha ambapo napata pesa za kulisha familia.”
Mnamo 2015, kama rais wa Nigeria,
Buhari alitangaza mali yake, akisema ana nyumba tano na nyumba mbili za udongo.