Watu wanashiriki maandamano dhidi ya mashambulizi ya Marekani dhidi ya Venezuela katika jiji la New York, Marekani, Januari 3, 2026. (Xinhua/Zhang Fengguo)
Wataalamu na vyombo vya habari vya Amerika ya Kusini wanaamini kuwa hatua ya Marekani dhidi ya Venezuela inalenga kuleta “athari ya kutisha” ili kuzuia nchi za eneo hilo, na kwamba ni toleo lililoboreshwa la “Itikadi ya Monroe.”
Baada ya jeshi la Marekani kuivamia Venezuela na kumkamata kwa nguvu Rais wa Venezuela Nicolas Maduro pamoja na mke wake Jumamosi, Rais wa Marekani Donald Trump alitangaza baadaye siku hiyo kuwa Marekani ita “endesha” taifa hilo la Amerika Kusini.
Mashambulizi ya Marekani dhidi ya Venezuela na kile kinachoelezwa kuwa “mpango wa usimamizi,” kama wachambuzi wanavyosema, kimsingi ni uthibitisho wa mpango wake wa kupanua “Itikadi ya Donroe” — toleo la Itikadi ya Monroe lililorekebishwa na Trump, linalolenga kudhibiti Ulimwengu wa Magharibi na kunyakua rasilimali zake.
“KUENDESHA” AU KUNYAKUA VENEZUELA
Trump aliambia mkutano wa waandishi wa habari Jumamosi kuwa Marekani itaunda kikundi kazi chenye wanadiplomasia na wanajeshi ili “kuendesha” Venezuela hadi kufikiwa kwa “mpito salama, unaofaa na wa busara.”
Pia alitishia kuwa Marekani “haiogopi” kuweka wanajeshi ardhini na itazindua wimbi la pili, kubwa zaidi, la mashambulizi dhidi ya Venezuela endapo itahitajika.
Ingawa mpango mahsusi bado haujawekwa wazi, kile kinachoitwa “kuendesha” na Marekani kimsingi ni jaribio la kuingilia moja kwa moja masuala ya Venezuela kupitia udanganyifu wa kisiasa na udhibiti wa rasilimali, wataalamu wamesema.
Allan Fajardo, mwanasosholojia katika Chuo Kikuu cha Kitaifa cha Uhuru cha Honduras, aliiambia Xinhua kuwa kuna uwezekano mbili kuhusu kile kinachoitwa “usimamizi wa mpito” wa Marekani.
Mojawapo ni kudumisha serikali na mfumo wa taasisi wa sasa wa Venezuela kwa sura ya nje, huku ikiendelea kuingilia masuala ya ndani ya nchi hiyo kupitia shinikizo la kisiasa na kiuchumi.
Njia nyingine inayowezekana ni kuunda moja kwa moja utawala unaounga mkono Marekani, bila hata kuondoa uwezekano wa uingiliaji mkubwa zaidi wa kijeshi na uvamizi wa eneo la Venezuela siku zijazo, alisema.
Trump pia alitaja katika mkutano wa waandishi wa habari kuwa makampuni makubwa ya mafuta ya Marekani yataingia Venezuela kukarabati miundombinu ya mafuta iliyochakaa sana na kuanza kuzalisha mapato.
Picha ya skrini kutoka kwa video iliyotolewa na Ikulu inaonyesha Rais wa Marekani Donald Trump akizungumza na waandishi wa habari katika jumba la Mar-a-Lago, Palm Beach, Florida, Marekani, Januari 3, 2026. Trump alisema uvamizi wa Marekani ulilenga “ngome ya kijeshi iliyoimarishwa sana katikati ya Caracas” ili kumkamata Maduro. (Xinhua)
Cao Ting, mkurugenzi wa Kituo cha Utafiti wa Amerika ya Kusini katika Chuo Kikuu cha Fudan, alisema kuwa kwa kuzingatia mtindo wa mara kwa mara wa utawala wa Trump, lengo lake la kimkakati huenda likawa kudhibiti mhimili wa mafuta wa Venezuela kwa kuunda mawakala wanaounga mkono Marekani nchini humo, bila kujihusisha na uvamizi wa muda mrefu.
Mfumo huu wa kile kinachoitwa “kuendesha” haujikita katika kuboresha maisha ya wananchi au kujenga upya nchi, bali katika kunyakua rasilimali, alisema Jaime Tamayo, mtaalamu wa mahusiano ya kimataifa na sayansi ya siasa kutoka Chuo Kikuu cha Guadalajara.
Hatua hiyo itasababisha kudhoofika kwa uwezo wa utawala wa Venezuela, kutenganishwa kwa usimamizi wa kiraia na usalama, kuzorota kwa usalama wa umma, na kuibuka kwa vurugu, wasomi wamesema.
VENEZUELA BAADA YA MADURO
Kwa mujibu wa Katiba ya Venezuela, endapo rais atakuwa “hayupo kabisa,” mamlaka huhamishiwa kwa makamu wa rais na uchaguzi mkuu hufanyika ndani ya siku 30.
Hata hivyo, Mahakama Kuu ya Haki ya Venezuela haikutangaza kuwa Maduro “hayupo kabisa,” ingawa ilimwagiza Makamu wa Rais Delcy Rodriguez kuchukua mara moja nafasi ya rais kaimu baada ya kukamatwa kwa Maduro. Kulingana na uchambuzi wa vyombo vya habari, hali hiyo inaashiria kuwa huenda uchaguzi mkuu usifanyike ndani ya siku 30.
Wataalamu wanaamini kuwa Rodriguez na kaka yake kwa sasa ni wawakilishi muhimu wa nguvu za mrengo wa kushoto, zenye misimamo ya wastani kwa kiasi fulani.
Katika hotuba ya televisheni Jumamosi, Rodriguez alichukua msimamo mkali dhidi ya Marekani, akilaani hatua zake kama uchokozi wa kijeshi usio na kifani na kusema Venezuela haitakuwa kamwe koloni ya nchi yoyote au mtumwa wa himaya yoyote, licha ya madai ya awali ya Trump kwamba aliahidi kufanya kile ambacho Marekani inataka.
Tamayo anaamini kuwa nguvu za kisiasa za mrengo wa kushoto nchini Venezuela na msingi wake wa kijamii bado ni imara kwa kiasi kikubwa, jambo linaloifanya iwe vigumu kwa Marekani kubadili muundo wa kisiasa wa nchi hiyo kwa muda mfupi. Huenda ikachagua mkakati wa kuchochea migawanyiko ili kuvutia baadhi ya viongozi wa juu wa kisiasa au kijeshi nchini Venezuela.
AMERIKA YA KUSINI KATIKA TAHADHARI KUBWA
“Leo ni Venezuela, kesho inaweza kuwa mtu mwingine yeyote,” alisema Rais wa Chile Gabriel Boric Jumamosi, akitoa tahadhari kwa nchi za Amerika ya Kusini kuhusu uingiliaji wa kihegemonia wa Marekani.
Wataalamu na vyombo vya habari vya Amerika ya Kusini wanaamini kuwa hatua ya Marekani dhidi ya Venezuela inalenga kuleta “athari ya kutisha” ili kuzuia nchi za eneo hilo, na kwamba ni toleo lililoboreshwa la “Itikadi ya Monroe.”
Watu wanashiriki maandamano dhidi ya mashambulizi ya Marekani dhidi ya Venezuela katika jiji la New York, Marekani, Januari 3, 2026. (Xinhua/Zhang Fengguo)
Jose Ignacio Martinez, mtaalamu wa mahusiano ya kimataifa kutoka Chuo Kikuu cha Kitaifa cha Uhuru cha Mexico, alisema kuwa Washington inaonyesha mantiki yake ya mabavu ya kuamua kiholela ni nani anaweza kuwa rais na ni nchi ipi ni “halali,” huku ikiziita kwa urahisi nchi na viongozi husika kuwa “magaidi,” “wauzaji wa dawa za kulevya,” au “madikteta.”
Viongozi wa Brazil, Mexico, Cuba, Honduras na Chile, miongoni mwa wengine, wamelaani hadharani hatua za Marekani na kuitaka jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua za haraka.
Rais wa Brazil Luiz Inacio Lula da Silva alilaani vitendo vya jeshi la Marekani kuwa “visivyokubalika,” akisema vilikiuka uhuru wa Venezuela na kuweka mfano hatari.
Hatua za Marekani zimegusa kiini cha uhuru wa kitaifa na zimeibua wasiwasi hata miongoni mwa baadhi ya makundi ya upinzani nchini Venezuela. Chini ya shinikizo linaloongezeka, nchi za Amerika ya Kusini huenda zikatamani mshikamano na kujitegemea zaidi ili kukabiliana na hegemoni, kulingana na uchambuzi wa vyombo vya habari vya eneo hilo.



