
MAHAKAMA kuu ya Bungoma imetoa uamuzi wa kipekee na wa kushangaza kuhusu kesi ambapo wanaume wawili walikuwa wanazozania haki ya kulea watoto baada ya mama yao kufa.
Mahakama hiyo ilitoa uamuzi ulioshangaza baadhi ya watu
kutoka jamii hiyo wakati iliamuru kwamba baba wa kambo ndiye mwenye haki
stahiki ya kuishi na watoto na wala si baba mzazi.
Kwa mujibu wa kesi hiyo, watoto wawili waliokuwa wanazozaniwa
na kina baba wawili walifiwa na mama yao mnamo 2021.
Baada ya kumzika mama, baba mzazi alijitokeza akiwa amejihami
na vyeti vyao vya kuzaliwa, mpango wa bima ya elimu na uthibitisho wa kuweza
kuwakimu kielimu.
Hata hivyo, watoto walidinda kumkubali na kusimama kidete na
baba wa kambo, jambo lililopelekea kesi hiyo kuhamishiwa mahakamani.
“Watoto hao walitoa
ushahidi kuwa hawakujua mshtaki (baba mzazi) ni nani kwani hawakuwahi kumuona
hapo awali na walipendelea kusalia chini ya malezi ya mshtakiwa (baba wa
kambo),” ilisomeka hukumu hiyo kwa sehemu.
Mahakama iliarifiwa kwamba baba wa kambo alikuwa ameishi na
watoto hao kwa takribani miaka 10 na japo ilithibitisha kwamba mshtaki ndiye
alikuwa baba mzazi, iliamuru baba wa kambo kuendelea kuishi na kuwalea watoto
hao.
Wakati wanaume wote wawili walipata hali ya malezi kwa watoto,
mahakama ilimpa baba wa kambo haki kamili, huku baba mzazi akitakiwa
kuwatembelea tu mara moja moja.
Majukumu yaligawanywa kwa baba mzazi kugharamia matibabu na
ada za shule huku baba wa kambo akitakiwa kushughulikia huduma za kila siku kwa
watoto.