
MAHAKAMA ya Upeo nchini Uingereza imetangaza kuwa ufafanuzi wa mwanamke unatokana na jinsia ya kibaolojia katika uamuzi uliotajwa kuwa wa kihistoria katika taifa hilo.
Lord Hodge alisema kuwa majaji watano
wa Mahakama ya Upeo waliamua kwa kauli moja kwamba 'maneno mwanamke na jinsia
katika Sheria ya Usawa yanarejelea 'mwanamke wa kibaolojia na jinsia ya
kibaolojia'.
Hata hivyo, alisisitiza kuwa sheria bado
inawapa watu waliobadili jinsia ulinzi dhidi ya ubaguzi.
Katika uamuzi wa kurasa 88, majaji
walisema: 'Ufafanuzi wa jinsia katika Sheria ya Usawa wa 2010 unaweka wazi
kwamba dhana ya jinsia haina maana, mtu ni mwanamke au mwanaume.'
Uamuzi huo unaweza kuwa na athari kubwa
juu ya jinsi haki za kijinsia zinavyotumika, pamoja na jinsi nafasi za wanawake
pekee zinaruhusiwa kufanya kazi haswa katika taifa hilo.
Uamuzi huo unaashiria hitimisho la vita
vya kisheria vya muda mrefu kati ya serikali ya Uskoti na kikundi cha wanawake
kuhusu ufafanuzi wa 'mwanamke' katika sheria ya Uskoti inayoamuru asilimia 50
ya uwakilishi wa wanawake kwenye bodi za umma.
Kesi hiyo ilihusu iwapo mtu aliye na
cheti cha utambuzi wa kijinsia anayetambua jinsia yake kama mwanamke anafaa
kuchukuliwa kama mwanamke chini ya Sheria ya Usawa ya 2010.
Serikali ya Uskoti ilisema kuwa watu
kama hao wana haki ya kulindwa kulingana na jinsia, wakati kikundi cha kampeni
cha For Women Scotland (FWS) kilidai kuwa inafaa kutumika kwa watu ambao
wamezaliwa wakiwa wanawake pekee.
Akitoa uamuzi wa mahakama, Lord Hodge
alisema: ‘Uamuzi wa pamoja wa mahakama hii ni kwamba maneno ‘mwanamke’ na
‘jinsia’ katika Sheria ya Usawa ya 2010 yanarejelea mwanamke wa kibaolojia na
jinsia ya kibayolojia.’
Hukumu hiyo ilisherehekewa na mashirika
ya kutetea haki za wanawake, ambao walishangilia nje ya mahakama, walifungua
chupa ya shampeni na kuvunja wimbo baada ya uamuzi huo kutolewa.