Mbunge wa Embakasi ya mashariki Babu Owino ametangaza kuwa ni lazima katiba itabadilishwa.
Kupitia kurasa zake kwenye mitandao ya kijamii ya Facebook na Twitter, mbunge huyo anayekumbwa na sarakasi si haba siasani amesema hawatorudi nyuma kwenye nia yao ya kubadilisha katiba kupitia mswada wa BBI.
Babu ametangaza matamshi haya siku moja baada ya mahakama kuu ya Kenya kutupilia mbali mchakato mzima wa BBI.
“Tutabadilisha katiba majaji wapende wasipende. Muswada huo unajali maslahi ya Wakenya.” Babu aliandika kwenye akaunti yake ya Twitter siku ya Ijumaa.
We will change the constitution whether the judges like it or not.The document is for the best interest of Kenyans.
— Babu Owino (@HEBabuOwino) May 14, 2021
Siku ya Alhamisi, mahakama ilikosoa hatua ya Rais Kenyatta kuongoza mchakato wa BBI huku majaji wakidai kuwa shughuli hiyo ilifaa kumilikiwa na wananchi na wala sio rais mwenyewe.
Majaji hao pia walikosoa hoja ya kuongeza maeneo bunge sabini huku wakiashiria kuwa kisheria hiyo ni kazi ya tume la IEBC wala sio jopo liliteuliwa na Rais.
Babu Owino ambaye ni mwandani mkubwa wa kinara wa ODM, Raila Odinga amekuwa kwenye mstari wa mbele katika kupigia debe mchakato wa BBI.
Mbunge huyo wa mara ya kwanza na aliyekuwa kiongozi wa muungano wa wanafunzi wa chuo kikuu cha Nairobi(UON) kwa muda mrefu anajulikana kuwa na ujasiri mwingi anapoongea.