logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Raia 7 wa kigeni walioingiza Kenya heroini ya Sh1.3bn kufungwa maisha

Hii ilikuwa hukumu ya kihistoria kwa walanguzi wa dawa za kulevya nchini Kenya.

image
na

Habari10 March 2023 - 14:05

Muhtasari


• Wakenya watatu, Khalid Agil Mohamed, Mohamed Osman Ahmed, na Maur Bwanamaka waliachiliwa kwa sababu walikodiwa tu kupakuwa meli hiyo baada ya kutia nanga bandarini Mombasa.

Raia 7 wa kigeni walioingiza Kenya heroin ya Sh1.3bn wahukumiwa kifungo cha maisha Picha: HANDOUT

Mahakama mjini Mombasa siku ya Ijumaa iliwahukumu maisha raia sita wa Pakistani na mmoja wa Iran walioingiza Kenya dawa za kulevya aina ya heroin zenye thamani ya shilingi bilioni 1.3 kupitia Bahari Hindi mwezi Julai 2014.

Akitoa hukumu hiyo ya Kihistoria hakimu mkuu wa Mombasa Martha Mutuku pia aliwatoza faini ya Shilingi milioni 3.9 kila mmoja pamoja na kifungo hicho kutumikia mwaka mmoja gerezani ikiwa hawatalipa faini hiyo.  

Mwezi Februari, mahakama iliwapata raia hao wa kigeni walionaswa ndani ya meli na hatia ya kusafirisha kilo 377.2 za heroin, zenye thamani ya Shilingi 1.3 bilioni, na lita 33,200 za heroin, zenye thamani ya Shilingi milioni 189.

Upande wa mashtaka uliongozwa na Naibu mkurugenzi wa mashtaka ya umma Alexander Muteti, akisaidiwa na Wakili Mkuu wa Mashtaka Peris Bosibori.

Sita hao ni Mohamed Saleh, Yakoob Ibrahim, Saleem Muhammad, Bhatti Abdulghafour, Baksh Moula, na Pak Abdolghaffer. Wakenya watatu, Khalid Agil Mohamed, Mohamed Osman Ahmed, na Maur Bwanamaka waliachiliwa kwa sababu walikodiwa tu kupakuwa meli hiyo baada ya kutia nanga bandarini Mombasa.

Mahakama ilisema kuwa ushahidi na vielelezo vilivyotolewa viliwaweka wageni hao katikati ya uhalifu na kubaini kuwa dawa hizo zilifichwa kwa uangalifu ndani ya meli yao jambo ambalo lilichukua siku za upelelezi kuzigundua.

Zaidi ya hayo, mahakama ilisema kuwa kubomolewa kwa meli ya MV Amin Darya hakukuwa na umuhimu kwa kesi hiyo kwa sababu kulitokea baada ya kuwepo kwa nyaraka za kutosha za eneo la tukio na kunaswa kwa dawa na kupima kuthibitisha.

Kukusanya na kuhifadhi ushahidi kulifanyika kwa mujibu wa sheria. Meli hiyo kwa jina Al Noor, ililipuliwa saa mwendo wa saa kumi jioni katika eneo linalojulikana kama Delta-16, ambalo limetengwa kwa ajili ya kurusha vilipuzi ndani ya eneo la maji ya Kenya, na kulipua.

Moshi ulitoka kutokana na mlipuko huo, ambao ulififia ndani ya dakika moja.  Eneo la mlipuko ni kama maili 10 kutoka eneo la karibu la ardhi.

Kumekuwa na ongezeko la kiasi cha heroini zinazouzwa Afrika Mashariki katika miaka ya hivi karibuni, kulingana na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya dawa za Kulevya na Uhalifu.

Dawa hizo kwa kawaida husafirishwa kutoka Pakistan na Iran hadi Afrika Mashariki, inayojulikana kwa mipaka yake inayovuja na ufuatiliaji dhaifu wa baharini, na kuendelea hadi Ulaya.

Mnamo Aprili meli ya kivita ya Australia ilinasa zaidi ya tani moja ya heroini yenye thamani ya dola milioni 268 kutoka kwa jahazi katika maji ya Kenya.

MHARIRI:  DAVIS OJIAMBO.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved