logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Kisa tata cha kutoweka kwa msusi Jane Mwende, polisi wachunguza

Kufikia sasa polisi  wamewakamata washukiwa wawili ambao wanadaiwa kuhusika na kutoweka kwa Jane Mwende.

image
na

Makala11 September 2023 - 04:11

Muhtasari


• Kufikia sasa polisi  wamewakamata washukiwa wawili ambao wanadaiwa kuhusika na kutoweka kwa Jane Mwende.

•Washukiwa hao walikamatwa Jumamosi jioni baada ya polisi kupata taarifa kuwa, Mwende angetoweka kwa sababu ya penzi. 

Jane Mwende/facebook

Kisa cha kutoweka kwa Jane Mwende, ambaye ni msusi katika eneo la Mlolongo sasa kimeibua maswali chungu nzima.

Maafisa wa polisi katika eneo la Mlolongo, wameanzisha uchunguzi ili kubaini kiini cha kutoweka kwa Jane, mwanamke mwenye umri wa miaka 28 ambaye hajaonekana tangu mnamo Agosti 25 baada ya kupigiwa simu.

Kufuatia uchunguzi , polisi  wamewakamata washukiwa wawili ambao wanadaiwa kuhusika na kutoweka kwa mwanadada huyo.

Washukiwa hao walikamatwa Jumamosi jioni baada ya polisi kupata taarifa kuwa, mwende huenda alitoweka kwa sababu ya penzi la mtu mmoja anayefahamika kama Januaris Musau almaarufu Shady. Mwanamke mwingine katika eneo hilo anayetambulika kama Phylis Mbithi anafuatiliwa na polisi.

Kufikia sasa polisi wanawasaka washukiwa wengine wawili, ambao wanashukiwa kuhusika na kutoweka kwa Jane Mwende.

Mnamo Agosti 25, Mwende alikua na shughuli nyingi za kutoa huduma katika saluni ya urembo na vipodozi ambapo alipokea simu.

Wenzake katika saluni hiyo wanasema alipokea simu kutoka kwa nambari isiyojulikana, na alipotoka nje kuijibu hakurudi tena.

Winnie Munyau,mmoja wa wafanya kazi katika saluni hiyo, alisema hawajawai kumuona tangu alipotoka kujibu simu walioichukulia kuwa ya mteja.

"Alipokea simu ikionekana kutoka kwa mteja na akatoka nje.Hatujawahi kumuona tangu wakati huo, na wala hakuja kazini siku iliyofuata,"

Familia na marafiki wamesema wameingia katika vituo vingi vya polisi, hospitali na vyumba vya kuhifadhia maiti wakimtafuta bila kufanikiwa.

Jennifer Mwende, Mfanyakazi mwenza aliongeza kusema;

"Hakutuambiwa chochote, alitoka akizungumza na simu, na hiyo siku kulikuwa na hitilafu ya umeme hivyo tukadhani simu yake ilikua imezima tukaamua kumsubiri ila hakurudi,"

Hali ya shaka ilitanda wakati ambapo Mwende hakurejea kazini asubuhi iliyofuata, aidha maji yalizidi unga wakati ambapo hakuenda kumchukua mwanawe kutoka shuleni.

Kufikia sasa Mwende, hajulikani aliko, polisi wakiahidi uchunguzi wa kina kubaini aliko.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved