Aliyekuwa Rais Uhuru Kenyatta amewaomboleza bosi wa zamani wa polisi King'ori Mwangi na mshikilizi wa rekodi ya dunia ya mbio za Marathon Kelvin Kiptum.
Katika taarifa yake, Rais huyo wa zamani alimkumbuka King'ori kama mtu aliyeonyesha ustadi mkubwa wa uongozi, uadilifu na kujitolea katika utumishi.
Uhuru alisema taaluma yake na kujitolea kwake katika huduma kulimfanya kupanda cheo tangu alipojiunga na Jeshi la Polisi la Kenya mwaka wa 1988 hadi kustaafu kwake 2022 katika wadhifa wake wa mwisho katika Wizara ya Mambo ya Nje.
King'ori alifariki Jumapili, Februari 11 katika hospitali moja jijini Nairobi alikokuwa amelazwa.
Familia yake ilituma ujumbe kwa marafiki zake kutangaza kifo chake.
“Tungependa kufahamisha umma kuhusu kifo cha Bw Kingori Mwangi, afisa wa polisi aliyestaafu. Kingori amefariki leo asubuhi katika hospitali ya Nairobi alikokuwa akipokea matibabu. Familia itasasisha umma kuhusu mipango ya mazishi. Kingori Mwangi Family” ulisomeka ujumbe huo.
Kiongozi huyo wa zamani wa nchi pia aliwapa pole wadau wa michezo kufuatia kifo cha Kelvin Kiptum ambaye alikuwa mshikilizi wa rekodi ya dunia ya mbio za marathoni za wanaume.
Alisifu mafanikio ya Kiptum, hasa kuwa mwanamume wa kwanza kuwahi kumaliza mbio za marathon chini ya saa mbili na dakika moja.
"Bwana Mwenyezi azipe familia zote mbili neema na ujasiri katika kipindi hiki kigumu," Uhuru alisema.
Kiptum na kocha wake raia wa Rwanda Gervais Hakizimana walifariki katika ajali mbaya ya barabarani Jumapili usiku katika eneo la Kaptagat kando ya barabara ya Elgeyo Marakwet-Ravine.
Inasemekana kuwa Kiptum ndiye aliyekuwa akiendesha gari lililokuwa likielekea Eldoret ajali hiyo ilipotokea.
“Ajali hiyo ilitokea majira ya saa 11 jioni. Gari hilo lilikuwa na watu watatu, wawili walifariki papo hapo huku mmoja akipelekwa hospitalini,” kamanda wa kaunti ya Elgeyo Marakwet Peter Mulinge alisema.
